Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?

Ni siku nyingine nzuri sana ya leo, ambapo tumepata nafasi bora na ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KAULI CHANYA YA KUIANZA SIKU…

Tunaishi kwenye dunia ambayo mambo hasi yanapewa kipaumbele kuliko mambo chanya.

Kila mtu anakazana kuiangalia upande hasi na mbaya wa kila jambo.

Hii ni hali hatari sana kwa sababu ukishakuwa unaegemea upande hasi, huwezi kuziona fursa nzuri za mafanikio na kuzitumia.

Hivyo unahitaji kuchukua hatua za makusudi za kuondokana na hali hizo hasi.

Na hatua unazohitaji kuchukua ni kuwa na kauli chanya ya kuianza siku yako.

Kauli hii unaiandika na kujiambia kila unapoamka, unakiri kauli hiyo chanya na kuipokea siku yako kama siku bora na ya mafanikio.

Unaweza kutengeneza kauli yoyote inayokufaa wewe.

Au unaweza kutumia kauli yetu chanya ya KISIMA CHA MAARIFA. Ambayo ni kama ifuatavyo;

Leo ni siku bora na ya kipekee sana kwangu, nakwenda kuweka juhudi kubwa na nategemea kupata matokeo makubwa. Ni kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA nakwenda kuleta tofauti kwenye maisha yangu na ya wengine.

Andika na jiambie kauli hii kila siku, ukiikiri kuwa yako na mwongozo wa maisha yako.

Unaweza kuona ni kauli ndogo, lakini itakuwa na matokeo ya tofauti sana kwako, ukilinganisha na dunia inayokutaka uwe hasi.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,

MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.

www.kisimachamaarifa.co.tz