Habari za leo rafiki yangu?

Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo, nafasi ya kipekee uliyoipata, ambayo kama utaitumia vizuri unaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

Nafasi hii uliyoipata leo, usiichukulie kirahisi, wapo wengi waliokuwa na mipango mikubwa leo, lakini hawajapata nafasi nzuri kama uliyopata wewe. Labda wameshakamilisha safari yao hapa duniani au wapo kwenye hali mbaya kiasi kwamba hawawezi kufanya kile walichokuwa wamepanga kufanya.

Leo napenda nikukumbushe jambo moja muhimu sana rafiki yangu, na ninakukumbusha kwa sababu watu tumekuwa tunajisahaulisha hili kila wakati, na jamii inapenda tusahau pia.

Jambo ninalotaka kukukumbusha ni kwamba, matokeo unayopata sasa ni sawa sawa na uwekezaji uliofanya kwenye kila eneo la maisha yako.

Kitu ambacho wengi wanaweza kushangaa ni kwamba kila kitu kinategemea uwekezaji. Hapa hatumaanishi fedha pekee, bali uwekezaji unafanyika mpaka unapata matokeo fulani.

Hivyo matokeo tunayopata kwenye kila eneo la maisha yetu ni matokeo ya uwekezaji ambao tumefanya.

Yapo mambo mengi tunayopaswa kuwekeza kwenye kila eneo la maisha yetu ili tuweze kupata matokeo mazuri.

Muda ni kitu kikubwa cha kuwekeza, hakuna matokeo yoyote mazuri tunayoweza kuyapata kama hatuweki muda wa kutosha kwenye chochote kile tunachofanya kwenye maisha yetu. Iwe ni kazi, biashara, afya, mahusiano n.k. muda unahusika sana, sana.

Lakini wengi wamekuwa wanalaghaiwa kwamba kuna namna ya kupita mkato, kupunguza muda unaopaswa kuwekwa na kupata matokeo makubwa ndani ya muda mfupi. Ni kweli, unaweza kukatisha muda unaopaswa kutumia, lakini matokeo utakayopata, hayatadumu kwa muda mrefu.

mafanikio yanahitaji muda

Kazi ni kitu kingine muhimu sana unapaswa kuwekeza, kwenye kila eneo la amisha yako. Unahitaji kuweka kazi hasa, kuweka juhudi, kwenda hatua ya ziada, kufanya zaidi ya unavyotegemewa kufanya. Kazi ndiyo inaleta matokeo ya tofauti, ndiyo inabadili hali ya mambo na kufanya hali mbaya kuwa bora zaidi.

SOMA; Tatua Changamoto Hizi Mapema Ili Zisikuzuie Kufanikiwa.

Hapa napo watu wamedanganywa sana, kwamba unaweza kupata matokeo makubwa, bila ya kuweka kazi kubwa. Na watu wanakimbilia njia hizo, wanaishia kupoteza muda wasipate matokeo hayo, na hata wakiyapata, hayadumu kwa muda mrefu. Au yanakuwa siyo halali na hivyo kuwasumbua.

Imani ni kitu unachopaswa kuwekeza kwenye kila unachofanya, kama huamini, bila ya shaka yoyote kwenye kile unachofanya, unapoteza tu muda wako. Kwa sababu imani ndiyo itakayokuwezesha kupiga hatua licha ya vikwazo na changamoto. Imani ndiyo inayokupa hamasa ya kupiga hatua zaidi. Na imani ndiyo inakuwezesha kuwashawishi wengine wakubaliane na wewe. Kama huna imani juu ya kile unafanya, kila mtu ataliona hilo na hakuna atakayekupa kile unachotaka.

Utashangaa sana mtu ana uzito wa mwili uliopitiliza, lakini anataka upungue haraka, bila ya kuweka muda wala kazi. Hivyo anahadaika kutumia dawa ambayo itampelekea kupunguza uzito, lakini baada ya muda anarudi kwenye uzito ule ule. Kwa sababu hajawekeza kile kinachopaswa kuwekezwa, kula kwa afya na kufanya mazoezi kila siku kwa muda mrefu.

Wengi sana wana changamoto za kifedha, lakini hawataki kuwekeza muda na kazi kwenye kutatua changamoto hizo, badala yake wanatafuta njia ya mkato, ambayo haihitaji muda wala kazi. Wengi wanakimbilia kukopa, kitu ambacho kinatengeneza tatizo kubwa zaidi baadaye. Wengine wanacheza kamari na bahati nasibu, wakiamini watashinda na kuagana kabisa na shida zao. Hapo bado wapo wale ambao wanakimbizana na kila aina ya fursa mpya, fursa inayoahidi mtu kupata mamilioni ya fedha kwa muda mfupi bila hata ya kufanya kazi kubwa.

Nikusihi tu rafiki yangu, ijue misingi ya mafanikio kwenye maisha, na ishi hiyo, usitetereke, misingi haijawahi kupinda hata siku moja. Kila kitu kinahitaji uwekezaji wa muda, kazi na imani ili kiweze kuleta matokeo mazuri.

SOMA; Mambo Matano(05) Unayopenda Sana Kufanya Ambayo Yanakuzuia Wewe Kufanikiwa Kwenye Maisha Yako.

Na ili kuwa upande salama mtu akikuambia NINA NJIA RAHISI YA KUPATA MATOKEO MAKUBWA HARAKA BILA YA KUFANYA KAZI KUBWA, mwambie asante sana na kimbia haraka mno. Usiendelee kumsikiliza ukifikiri njia yake labda ina usahihi fulani. Ukimpa tu nafasi, atakupoteza, kimbia haraka na endelea kuweka muda, kazi na imani kwenye kile unachofanya.

Unapata sawa sawa na unavyowekeza, achana na wale wanaotaka kukupotezea muda usiwekeze, wewe jiandae kabisa kuwekeza muda wa kutosha, kazi ya maana na imani isiyoyumbishwa kwenye kila unalofanya na hakika utakutana na mafanikio mchana kweupe kabisa.

Karibu tuwekeze kwenye kujifunza kwa kusoma kurasa kumi za kitabu kila siku, tembelea www.amkamtanzania.com/kurasa kupata maelezo kamili.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog