Mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii imempa kila mtu sauti, kila mtu sasa anaweza kuongea, kila mtu anaweza kutangaza chochote na kuwafikia watu wengi zaidi.

Kibiashara hili limeleta changamoto mpya kwa wateja. Wanasikia kelele nyingi sana kiasi kwamba wanashindwa kujua wachukue hatua gani. Pale kila mtu anapoongea na kuahidi mambo mazuri, wateja wanashindwa kujua wamwamini nani na kununua kwake.

kelele mtandaoni

Na hapa ndipo kilipo kilio cha chini chini cha wateja, huku wakitamani kitu kimoja muhimu sana kutoka kwako wewe kama mfanyabiashara.

Kwa kuwa tayari wateja wanamsikia kila mtu akisema, wanatamani sana mtu mmoja ambaye anaweza kuwahakikishia kwamba kile wanachoambiwa ni kweli. Kwamba kweli wakinunua bidhaa au huduma inayouzwa, itawawezesha kutimiza mahitaji au kutatua changamoto zao.

Mteja anaomba kabisa, japo hasemi, mtu ajitokeze, afunike hizo kelele za wengine kwa kumpa uhakika wa kile anachouza. Kumwonesha wengine walionunua na mambo yao yakawa mazuri. Kumpa uhakika kwamba kama hakitamfaa basi atakuwa hajapoteza fedha zake, kwani atasaidiwa au kupewa kinachomfaa na kama yote yatashindikana, basi kurejeshewa fedha alizolipia.

SOMA; BIASHARA LEO; Bidhaa Bora Haihitaji Punguzo La Bei…

Hichi ndiyo kilio cha wateja kwenye zama hizi tunazoishi. Angalia kwa biashara unayofanya, ni jinsi gani unaweza kutatua kilio hichi na kuwasaidia wateja, ambao watakuwa wako kwa muda mrefu.

Toa bidhaa au huduma ambayo kweli ina msaada kwa wateja wako, na kuwa karibu na wateja wako kwa changamoto yoyote wanayoweza kuipata kutokana na manunuzi waliyofanya kwako.

Nikukumbushe tu kwamba, muda wa mteja pia ni mdogo sana, hivyo unahitaji kuwa na mfumo bora wa kumwezesha yeye kukuamini na kununua kwako kwa muda mfupi atakaokusikiliza au kukufuatilia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog