Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Ni siku nyingine nzuri sana na ya kipekee ambapo tumepata fursa nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Leo tutafakari kuhusu KUJUA CHA KUFANYA NA KUFANYA UNACHOJUA…
Karibu kila mtu anajua anachopaswa kufanya, kwenye kila hali ya maisha yake, lakini ni wachache sana kufanya kile wanachojua wanapaswa kufanya.
Kila mtu ni rahisi kuwasema wengine wanapaswa kufanya nini, au wanakosea wapi kufanya, lakini wao hawapo tayari kufanya.
Wengine ni wagumu sana kushauriwa au kujifunza, hujiambia najua hayo yote, sina haja ya kujifunza tena, lakini hawafanyi kile wanachojua.
Watu wengi wanayajua yale ya msingi kwenye maisha, kazi, biashara, fedha, mahusiano, afya. Lakini cha kushangaza, hawafanyi kama ambavyo wangepaswa kufanya.
Ndiyo kuna changamoto ya ukosefu wa nidhamu, hivyo watu wanaweza kupanga lakini wakisikae chini na kufanya kwa uhalisia.
Lakini changamoto nyingine kubwa ni watu hawajaimbiwa au kujiimbia vya kutosha. Mtu anajifunza au kusema mara moja najua napaswa kufanya hivi, baada ya hapo maisha yanaingilia kati, changamoto nyingine zinamteka na kusahau kile ambacho alipaswa kufanya.
Hivyo watu wanahitaji kuimbiwa sana, kuambiwa tena na tena na tena. Wanahitaji kujiimbia wao wenyewe, kujiambia tena na tena na tena.
Hata kama unajua, kaa chini na jifunze, hata kama ulishasikia, sikiliza tena, hata kama ulishajikumbusha, jikumbushe tena
Hakuna maana ya kujua unachopaswa kufanya kama hutafanya kile unachojua.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.
hakika vipande hivi vinanifunza mambo mengi sana kocha, na pia zinanipa hamasa pale ninapochoka , Barikiwa sana
LikeLike
Karibu Loma.
LikeLike