Mwaka huu nimepata fursa ya kukutana na kuwasiliana na wadau mbalimbali ambao kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kupitia uwekezaji huu wa rasilimali ardhi na majengo. Wengi wao ni wabobezi na wazoefu wa miaka mingi kwenye uwekezaji huu barani Ulaya, Afrika na Australia. Yapo mambo kadhaa niliyojifunza kutoka kwao kwa nyakati tofauti niliokutana na kuwasiliana nao kwa ajili ya kubadilishana maarifa na uzoefu.

Wengi wa marafiki hawa wamewekeza kwenye majengo, kilimo, huduma za jamii na utoaji huduma ya ushauri kwenye mambo yanayohusu uwekezaji wa mali na ujenzi. Lakini kikubwa kilichonishtua ni kwamba hawa wenzetu wana upeo mkubwa wa kuziona fursa tulizonazo watanzania kuliko sisi wenyewe, jambo hili lilinifanya niwe mpole na kujiuliza maswali mengi ambayo baadhi nagundua kuwa tatizo letu kubwa lipo kwenye uwekezaji wa maarifa.

majengo32

Mkwamo mkubwa unaotukabili na kutukwamisha kwenye hatua mbalimbali kuelekea kwenye mafanikio yetu chanzo kikuu ni kukosa hamasa na maarifa sahihi juu ya jambo fulani tunalolipigania. Maarifa sahihi ni silaha kuu ya mafanikio ambayo ikitumika vizuri inabadilisha maisha yetu na jamii kuwa bora zaidi ya tulivyo sasa. Wengi wao wamepitia hatua tofauti za mafanikio, lakini walizingatia sana hizi hatua tano katika kuanza uwekezaji wao na kuwafikisha walipo sasa.

Hatua ya kwanza; Jipe Hamasa Na Jiwekee Malengo.

Hamasa ni msukumo wa ndani ya fikra juu ya jambo fulani, hamasa ni matokeo chanya ya mfumo wa fahamu katika utendaji kazi kwenye mwili. Katika maisha yetu ya kila siku yapo mambo mbalimbali ambayo tumeyapa kipaumbele zaidi ya mengine, hii inatokana na ufinyu wa matumizi ya rasilimali muda. Kujipa hamasa na kujiwekea malengo fulani kuhusu mafanikio yako ni njia pekee ya awali katika kupata ushindi kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo. Hakuna jambo rahisi kwenye uwekezaji huu, lakini haimaanishi kwamba haiwezekani wewe kutimiza malengo yako. Njia pekee ni wewe kutafakari na kujiwekea malengo makuu kuhusu aina gani ya uwekezaji utakaoufanya na mikakati madhubuti katika kukuwezesha kufikia mafanikio yako. Ukweli ni kwamba waliofanikiwa walikubali kupambana na aina zote za changamoto pasipo kukata tamaa na walifanya maamuzi yenye hamasa ya ushindi hatimaye kutimiza malengo yao.

SOMA; Hizi Ndizo Mbinu Bora Za Kuepuka Majanga Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

Hatua ya pili; Wekeza Kwenye Elimu Na Maarifa.

Hatua hii ni muhimu sana katika kuyafikia mafanikio yako, wekeza sana kwenye elimu na maarifa, fahamu kuwa elimu ni dira na maarifa ni silaha ya ushindi katika kuyafikia mafanikio yako.  Tunahitaji juhudi kubwa katika kuwekeza maarifa na elimu katika aina hii ya uwekezaji ili itusaidie kutuongoza na kufanya maamuzi sahihi yatakayotufikisha kwenye maisha ya ushindi. Pamoja na uwepo wa teknolojia ya mawasiliano bado wengi wetu haijatusaidia katika kuboresha maisha yetu na kutimiza malengo yetu ya kimafanikio. Ni muhimu sana tukafanya uamuzi wa kutumia teknolojia hii ya mawasiliano katika kujipatia elimu muhimu itakayo kutusaidia kuboresha maisha yetu ikiwemo kujifunza mbinu mbalimbali za kimafanikio. Weka utamaduni wa kuwatembelea marafiki na washauri, nunua vitabu na majarida, hudhuria semina na matamasha yanayohusu uwekezaji wa ardhi na majengo ili ujifunze mambo ya ziada na yaliyo nje ya ukomo wako wa kufikiri, hii itakuongezea maarifa na mtandao mpya wa wadau ambao ni mtaji katika kuyafikia mafanikio yako.

Hatua Ya Tatu; Zingatia Maono Na Weka Kwenye Matendo.

Utashi ulionao juu ya maono mahususi kuhusu maisha yako ndiyo utakao kusukuma na kuamua aina gani ya maisha unapaswa kuyaishi. Kuwa na malengo na maono makubwa  kuhusu mafanikio na maisha hugeuka kuwa hayana thamani pasipo kuweka matendo,  hili litabaki kuwa ni tatizo lako binafsi hata kama utaweka juhudi kubwa kwenye nidhamu ya kujifunza maarifa ya uwekezaji huu. Jifunze kuchukua hatua kwa kile unachojifunza ili kikusaidie kuboresha maisha yako na uwekezaji unaoufanya. Juhudi zako katika kuyatenda na kuyafanyia kazi mambo yote muhimu na kwa wakati sahihi ni mbinu bora ya kuyafikia mafanikio yako. Usisite wala usiruhusu hofu itawale fikra zako na kukuzuia kuchukua hatua kwenye mambo ya msingi ambayo ni muhimu katika kuboresha maisha yako na wengine wanaokuzunguka. Kabla hujafikilia kuahirisha maamuzi yako, fikiria hatua utakayoipoteza kuelekea mafanikio yako. Amua kutenda na anza leo ili uwe mwekezaji bora katika ardhi na majengo.

Hatua ya nne; Nidhamu Ya Fedha Na Muda.

Nidhamu ya fedha na muda ni tatizo kubwa kwa wengi wetu. Utamaduni na mfumo wa maisha yetu bado haujatuimarisha katika matumizi sahihi ya rasilimali fedha na muda, bado hatujajenga urafiki sahihi wa umuhimu wa matumizi ya muda na fedha katika kuboresha maisha yetu na kuyafikia mafanikio tunayopaswa kuyafikia kwa wakati. Ni muhimu kutambua kuwa muda na fedha ni rasilimali muhimu inayopaswa kuwekewa mikakati madhubuti ya matumizi katika kuimarisha uwekezaji wa ardhi na majengo. Muda sahihi wa kuanza uwekezaji ni leo, usisubiri ukamilike kwa kila kitu bali anza na hatua ya kwanza huku ukijiandaa na mambo mengine, nidhamu ya matumizi ya fedha, mipango sahihi ya uwekezaji na kujiwekea akiba ni mbinu muhimu sana itakayokufanya uwe imara katika kukua kibiashara na uwekezaji wa ardhi na majengo. Uwekezaji huu unahitaji sana kuwa na nidhamu kubwa ya mipango ili ukuletee faida na mafanikio makubwa ndani ya muda muafaka. Anza leo kujiwekea akiba kwa kiasi unachopata, anza leo kuwasiliana na wadau wa ardhi na majengo, weka bidii ya kuwa na nidhamu ya matumizi ya muda kwa mambo ya msingi ambayo yataboresha maisha yako.

SOMA; Fahamu Chanzo Kikuu Cha Fangasi Kwenye Majengo Na Mbinu Za Kuziepuka.

Hatua Ya Tano; Matumizi Bora Ya Wataalamu.

Mfumo wa maisha ya mwanadamu unabadilika kila siku mpya inapokuja, mabadiliko yanapokuja ni vizuri ukajiandaa kuyapokea na kuyachuja ili uwe tayari kuendana nayo pasipo kukuletea madhara. Ni vigumu sana kupambana na mabadiliko ya mifumo ya dunia, lakini kuna baadhi ya marafiki bado wameshikilia mifumo ambayo haipo, na kama ipo ni vigumu sana kusogea popote au itawaletea madhara. Biashara na uwekezaji wa sasa unafanyika katika mifumo na mbinu za kisasa sana, wakati tulionao kila jambo lina wajuzi wake wenye maarifa ya kutosha. Ni muhimu sana kutumia wataalamu kwa mambo ambayo huna uelewa nayo ili wakusaidie kukupa mwongozo sahihi kuelekea mafanikio yako. Epuka hasara na migogoro isiyo na sababu kwa kufanya uwekezaji kwa kutumia mbinu za kisasa ikiwemo kutumia wataalamu. Usingoje mambo yaharibike ndipo uanze kulalamika na kutafuta usahihi wa mambo, itakugharimu sana tofauti na ungefanya hapo awali.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

 

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com