Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana na ya kipekee kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu UNAIANZAJE SIKU YAKO?
Rafiki yangu, kitu muhimu sana kwenye siku yako ni jinsi unavyoianza siku yako.
Wahenga waliona mbali sana waliposema NYOTA NJEMA HUONEKANA ASUBUHI…
Na hata walipokwenda mbali zaidi na kusema BIAHSARA NI ASUBUHI, JIONI MAHESABU, walijua kwa kina umuhimu wa mwanzo wa siku ambayo ni asubuhi.
Namna unavyoianza siku yako kunaathiri siku yako nzima.
Iwapo utainza siku ukiwa chanya, utakuwa na hamasa ya kufanya makubwa siku nzima.
Lakini ukiianza siku ukiwa hasi, siku yako itaisha ukijiuliza hivi muda leo umeenda wapi?
Unaianza siku ukiwa chanya iwapo utaianzia siku yako ndani yako, kwa kufanyia kazi MWILI, AKILI NA ROHO YAKO.
Ukiianza siku kwa kujifunza, kwa kujisomea kitabu kizuri, kusali na kutahajudi na kujisomea kitabu kizuri, unakuwa una silaha zote bora za kuiteka siku yako na kudhibiti muda wako.
Lakini ukiianzia siku yako nje yako, kwa kuanza kufuatilia mambo ambayo hayakuhusu, unakuwa hasi siku nzima. Siku nzima utakuwa unafanya mambo kwa mwitikio (REACTION) na siyo kwa mipango yako mwenyewe (ACTION).
Unaiharibu siku yako unapoianza kwa habari, kuperuzi mitandao ya kijamii na mawasiliano mengine ambayo yanakuonesha wengine wanafanya nini.
Na kinachoua siku yako zaidi ni pale unapochelewa kuianza siku yako, huku ukiwa hujaipangilia.
Uzuri ni kwamba, haya yote yapo ndani ya uwezo wako, kuianza siku chanya na kufanikiwa, au kuianza siku hasi na kuipoteza.
Ni wewe mwenyewe uamue unataka nini na uchukue hatua.
Neno langu kwako rafiki yangu, ianze siku yako vizuri, ianze ukiwa hasi, lisha akili yako, mwili wako na roho yako. Ianze siku mapema ukiwa umeipangilia na chukua hatua badala ya kusubiri kuitikia hatua za wengine.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.