Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu YUPO AMBAYE NI ZAIDI YAKO…
Chochote kile ambacho unafanya kwenye maisha, yupo ambaye ni zaidi yako.
Hata ungekuwa na fedha kiasi gani, yupo ambaye atakuwa na fedha zaidi yako.
Hata kwenye kipimo chochote cha maisha mazuri unachotumia, yupo ambaye maisha yake utaona ni mazuri zaidi yako.
Pamoja na hayo, bado watu tunapenda sana kupima maisha yetu kupitia wengine, na hii ni njia rahisi kabisa ya kujiangusha au kukata tamaa.
Pale unapokazana uwe namba moja au uwashinde wengine wote, unakuwa umejiandaa kuangushwa, umejiandaa kukata tamaa. Kwa sababu ni lengo gumu, ambalo huwezi kulifikia.
Kila unapopiga ngazi kwenye maisha yako, ndiyo unagundua kuna ngazi nyingine nyingi juu, na wapo watu ambao maisha yao ni bora kabisa kwenye ngazi hizo.
Wakati mwingine unaweza kuona kukimbizana na wale waliokuzidi ni jambo sahihi, la kukupeleka kwenye mafanikio zaidi.
Lakini hapo unapaswa kuwa makini sana, kwa sababu kama unashindana nao, ili uwe kama wao, umeshapoteza. Huwezi kuwa kama yeyote hapa duniani na ukaridhika.
Unaweza kuwa wewe pekee.
Hivyo unachopaswa kufanya ni kukazana kuwa wewe, kuwa bora zaidi leo kuliko jana, kupiga hatua zaidi. Lakini siyo kukazana kuwa kama mwingine yeyote.
Kama unaweza kupata hamasa kutoka kwa wengine inasaidia, lakini hakikisha hamasa hiyo ni ya kukazana kuwa wewe, na siyo kukazana kuwa kama wao, kujilinganisha nao.
Kwa sababu hata ukazane vipi, lazima atakuwepo ambaye ni zaidi yako.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.