Uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo umekuwa kivutio kikubwa kwa maelfu ya watanzania wa leo tofauti na wakati uliopita. Maelfu ya watanzania na wageni mbalimbali wanaendelea kuboresha maisha yao kupitia uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa kivutio kwa wengi kutokana na kuwa na sifa za kipekee katika uboreshaji na uendeshaji hata kufikia kuwa mwekezaji mwenye mafanikio. Fursa nyingi zilizopo kwenye ardhi na majengo zimetoa uwanja mpana kwa watu wote wenye nia na kiu ya mafanikio kuwa na aina tofauti ya matumizi ya rasilimali hizo ili kuboresha maisha yao binafsi na jamii inayowazunguka. Pamoja na hayo bado kuna idadi kubwa ya watu ambao wapo njia panda kwenye kufanya maamuzi ya uwekezaji, bado wapo kwenye utafiti kufahamu aina mbalimbali za uwekezaji na uwekezaji upi utakuwa wa faida kwao kabla ya kuwekeza popote. Hali hii ni matokeo chanya ya mwamko wa kimaendeleo wa kiuchumi na kifikra ambao unabadilisha maisha ya watanzania wengi kila siku mpya inapoingia.

majengo 33

Pamoja na hali tofauti za mabadiliko ya kiuchumi tunazopitia, uwekezaji wa ardhi na majengo bado umeendelea kuwa imara tofauti na uwekezaji mwingine, athari zake kwenye mtikisiko wa kiuchumi huwa ni mdogo ukilinganisha na uwekezaji mwingine. Hii ndiyo sababu ya wengi kuchagua kuwekeza kwenye ardhi na majengo na kuendelea kufurahia maisha yao ya kimafanikio katika hali zote za kiuchumi. Leo nitazungumzia sifa pekee utakazo nufaika nazo endapo utakuwa umewekeza kwenye ardhi na majengo ambazo ni tofauti au kuna unafuu zaidi dhidi ya uwekezaji mwingine.

Ni Rahisi Kuwekeza

Moja ya mambo yanayowavutia watu wengi ni urahisi wa mipango na mbinu za uwekezaji. Uwekezaji wa ardhi na majengo hauhitaji michakato mingi sana au ukaribu uliopitiliza. Ni rahisi ukawa mwekezaji wa ardhi na majengo huku ukijishughulisha na mambo mengine ya kimaisha na bado thamani ikawa kubwa pasipo kuwa na msongo wa mawazo kuhusu uwekezaji wako. Ni uwekezaji wa kuaminika na usalama wake ni mkubwa, ukitaka kuongeza mapato ni kitendo cha kuboresha aina hiyo ya uwekezaji tofauti na ulivyonunua, pia muda ni kitu kinachoongeza thamani, unaweza nunua kiwanja au nyumba leo lakini baada ya saa kadhaa mbele ukauza kwa thamani ya juu zaidi. Pia inatoa wigo mpana kwa mtu yeyote na wa kipato chochote na mahali popote na wakati wowote, ni kitendo cha wewe kuamua kuchagua na kuwekeza.

SOMA; Fahamu Hatua Tano (05) Muhimu Za Kuzingatia Kabla Hujaanza Kuwekeza Kwenye Ardhi Na Majengo.

Uhakika Wa Mapato.

Uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo ni uwekezaji ambao unatoa fursa za wewe kuwa na uhakika wa kipato na kujiimarisha zaidi kulingana na thamani ya uwekezaji wako. Pamoja na mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea kutokea bado athari zake ni ndogo sana kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo tofauti na uwekezaji mwingine, ni nadra sana kupata hasara ikiwa utakuwa makini, ni rahisi kujipatia mapato kwa njia ya mkopo au kupangisha kwa wengine na bado ukaendelea kuwa mwekezaji mwenye mafanikio ya kiuchumi hata kama hauna nguvu za kuendelea kuboresha zaidi. Mwalimu wangu aliwahi kusema kuwa “ardhi ndiyo pensheni yako ya uhakika, itakufaa hata uzee wako” akiwa na maana kuwa uwekezaji huu ni muhimu zaidi hasa kwa wote ambao wamejiajiri wenyewe na hawana utamaduni wa kujiwekea akiba, ni vema ukaanza kuwekeza sasa kwa kuwa utakufaa hata uzee wako, epuka msongo wa mawazo na furahia maisha kwa kuwa mwekezaji bora na mwenye mafanikio kwa kuanza na hicho kidogo ulichonacho sasa.

Unafuu Wa Kodi.

Pamoja na mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza kwenye uchumi na jamii kwa ujumla bado kuna fursa nyingi ambazo kila Mtanzania anapaswa kuzitumia katika kuboresha maisha yake kupitia rasilimali ardhi. Sera na sheria tulizonazo kwa sasa bado zimetoa unafuu na upendeleo mkubwa kwa wazawa kuhusu umiliki na matumizi ya rasilimali ardhi tofauti na uwekezaji mwingine, unafuu wa kodi ya ardhi na majengo bado ni mkubwa tofauti na uwekezaji mwingine, changamoto kubwa ipo kwenye usimamizi wa sera na sheria hizo katika kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na rasilimali ardhi. Hii ni fursa ambayo tunapaswa kuitumia ipasavyo katika kuboresha maisha yetu na vizazi vijavyo. Tafakari sana na amua leo kuanza harakati za kuboresha maisha yako.

Ni Mali Na Inakidhi Matumizi Binafsi.

Katika historia ya vizazi vilivyopita, ardhi na majengo haikuwa katika mfumo na mtazamo wa kibiashara kama ilivyo sasa bali ilikuwa kama hitaji muhimu la kibinadamu katika kukidhi mahitaji binafsi. Mabadiliko ya mifumo ya uchumi duniani imesababisha kuwa ni chanzo cha mapato kwa wale wote watakao tumia rasilimali ardhi katika kuboresha maisha ya wengine. Hii ndiyo faida ya pekee kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo tofauti na uwekezaji mwingine, ni mtaji kwa ajili ya shughuli nyingine za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Changamoto kubwa inayotukabili ni usimamizi hafifu wa mamlaka husika za kiserikali za kuhakikisha kuwa watu wake wanakuwa na makazi bora na kupangilia vema ukuaji wa miji na vijiji, hali inayowanyima watu wengi kupata huduma bora za kijamii na kukosa miundombinu rafiki ili waweze kuboresha rasilimali ardhi na majengo katika mifumo rasmi ya kiuchumi.

SOMA; Huu Ndiyo Uwekezaji Bora Kabisa Unaokufanya Wewe Kuwa Tajiri Kwenye Maisha Yako.

Huacha Alama Na Urithi Kwa Vizazi Vingine.

Wengi wa marafiki niliopata kukutana na kuwasiliana nao kuhusu Makala hizi walipata kujipongeza sana au kuwapongeza wazazi wao kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuamua kununua ardhi au kujenga. Kwao umekuwa msaada mkubwa sana kwenye mapito magumu ya kiuchumi yanapowakuta, wamejikuta wakitumia kuendesha na kuboresha maisha yao binafsi na sehemu kupangisha kwa wengine kama chanzo mbadala cha mapato. Hii ndiyo faida ya pekee kwenye uwekezaji huu, kitu pekee unachohitaji ni maarifa na kutenda ili kuijenga vizuri kesho yako na vizazi vyako. Hii ni alama na urithi pekee kwa jamii inayokuzunguka, hauhitaji kuwa na elimu kubwa sana kufanikiwa, ni mali inayoonekana mbele ya macho ya jamii, ni urithi kwa vizazi vyako na heshima itakayolinda utu wako pale itakapotumika kukuhifadhi wewe binafsi na muda huohuo kuwa sehemu ya kipato chako nyakati ngumu za kiuchumi utakazopitia. Tafakari kuhusu maisha yako binafsi na vizazi vyako, hakika utagundua kuwa uwekezaji rahisi, bora na muhimu ni ardhi na majengo.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com