KITABU; Socrates’ way : seven master keys to using your mind to the utmost / Ronald Gross.
UKURASA; 111 – 120.

Socrates anatufundisha kuhoji na kutoa changamoto kwa kila kitu. Anatuambie tuondoke kwenye gereza ambalo tumejifungia la kupokea kila kitu kama kilivyo.

Moja ya maeneo muhimu ya kuchukua hatua hizo ni kwa wale tunaowaita wataalamu.
Kwenye kila eneo la maisha yetu, kuna wataalamu wake.
Kwenye afya kuna wataalamu, kwenye biashara wapo wataalamu, kwenye ujenzi na kila eneo, wapo watu ambao wanaonekana ni wataalamu.
Watu wengi wamekuwa wakichukua maneno au ushauri wa wataalamu hao bila ya kuwahoji au kujihoji wao wenyewe. Wanabeba kitu kama kilivyo pale tu wanapoambiwa mtaalamu kasema hivyo.

Tunapaswa kuwatumia wataalamu kwa hekima sana. Kwa sababu wataalamu nao ni watu, wanaweza kukosea, lakini pia nao wana tamaa zao, na madhaifu yao mengine.
Katika kuwatumia vizuri wataalamu, yapo mambo haya mawili muhimu kufanya;

Moja; Chimba ndani kuwajua wataalamu na ushahidi wao.
Hapa unahoji ili kujua kweli iwapo wale unaowachukulia kama wataalamu ni wataalamu kweli.
Na hapo unaangalia ushahidi walionao, wataalamu wengi watakuambia tafiti zinasema. Hapo unahitaji kukagua tafiti hizo, kuona kama hazina makosa, kujua nani alifadhili tafiti hizo.
Kwa hatua hii utaweza kuona ukweli kwa uhalisia wake na siyo kwa kuambiwa.

Mbili; Chagua wataalamu unaoweza kuwaamini.
Kwa kuwa maisha yako yana maeneo mengi yanayoguswa na wataalamu mbalimbali, ni vigumu wewe kuweza kuchunguza kila kitu.
Hapa ndipo unapohitaji kuchagua wataalamu ambao utaweza kuwaamini ja kufanyia kazi ushauri wanaotoa.
Hapa unahitaji kuwa umewafuatilia kwa muda na kujiridhisha ile misingi wanayosimamia.
Lakini pia mara kwa mara chunguza na hoji, kuhakikisha upo upande wa ukweli.

Tusiogope kuhoji kwa sababu wataalamu ndiyo wamesema, una haki ya kuujua ukweli kabla hujafanya maamuzi muhimu kwako.

Kocha Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa