Let not your mind run on what you lack as much as on what you have already. – Marcus Aurelius

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi nyingine nzuri kwetu ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ULICHOKOSA NA ULICHONACHO….
Sisi binadamu wakati mwingine ni viumbe wa ajabu sana.
Mtu anaweza kuwa na vitu vingi vinavyokwenda vizuri kwake, ila kimoja au vichache vikawa haviendi vizuri, akasahau yale yote yanayokwenda vizuri na kukazana na yasiyokwenda vizuri.

Mtu anaweza kuwa na vitu vingi kwenye maisha yake, lakini akakosa vichache, na akili yake yote ikawa kwenye vile vichache alivyokosa.
Ni kawaida kwetu kukazana kufikiria kile tulichokosa kama ndiyo kikwazo kwa sisi kufanikiwa na kusahau kwamba kuna vitu vingi ambavyo tayari tunavyo na vinaweza kutusaidia sana.

Tunapokazana na kile ambacho hatuna, au ambacho hakiendi vizuri, ndivyo tunavyozidi kukosa na kuona maisha yatu hayana maana.
Lakini tukiangalia kile ambacho tayari tunacho, tunaona maisha yetu yana maana na tunaweza kupiga hatua zaidi.

Asubuhi ya leo, chukua kalamu na karatasi na orodhesha kila ulichonacho, au orodhesha vitu kumi ulivyonavyo, ambavyo ukivitumia vizuri vinakusogeza mbele.
Kwa kuangalia vitu hivyo, unapiga hatua kubwa kuliko kuangalia ulivyokosa.

Uwe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa