Nenda kwenye kazi au biashara yoyote, kusanya watu 100 bila ya mpangilio
maalumu, linganisha kipato wanachopata wote, utagundua kwamba wachache
wana kipato kikubwa, huku wengi wakiwa na kipato kidogo na cha kawaida.
Hili lipo kwenye kila eneo. Sasa wale wasiojua, wanachofanya wanawaangalia
wachache wanaofanya vizuri, wanaotengeneza kipato kikubwa na kusema ile
ndiyo fursa inayolipa.
Ukweli ni kwamba, popote unapoona watu wanatengeneza kipato kikubwa na
kufanikiwa, ni kwa sababu wameweza kujitengeneza na kuwa sumaku ya
fedha. Unawaona hao wachache kwa sababu wameshakuwa sumaku,
wanavutia kila senti inayokatiza karibu yao.
Na wewe pia unaweza kuwa sumaku ya fedha, kupitia chochote unachofanya.
Unachohitaji ili kuwa sumaku ya fedha, ni kuwa bora sana kwenye kile
unachofanya. Chochote unachofanya, kazana kuwa bora sana, kuwa bora
kuliko wengine wote wanaofanya kile unachofanya wewe.

Unapokuwa bora, fedha zinakufuata. Kwa sababu watu wanapenda kilicho
bora. Watu wanapokuwa na uhitaji mkubwa, wanataka kupata kile kilicho
bora. Hivyo unapokuwa bora, unapofanya kilicho bora, unakuwa umewapa
watu sababu ya kukuamini na kukutegemea wewe.

SOMA, # Ukurasa Wa 1028; Kataa Kutumiwa Na Wengine, Anza Kujitumia Mwenyewe……

Ukiwa bora wala hutahangaika kwamba fedha zinatoka wapi, fedha lazima zije,
kwa sababu umeshakuwa bora.
Tahadhari; unapokazana kuwa bora wapo watakaokukatisha tamaa na
kukusema vibaya. Hawa ni wale walioshindwa au ambao hawajawahi kuchukua
hatua kubwa kwenye maisha yao. Wapuuze, wewe kazana kuwa bora, hakuna
jingine muhimu zaidi ya hilo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea
http://www.mtaalamu.net/patablog