Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza maisha bora wanayostahili kuishi wanandoa katika karne ya 21 hivyo basi,  karibu tujifunze.

Ndoa ndiyo chimbuko la miito yote tunayoiona hapa duniani. Hatuwezi kuongezeka duniani kama hakuna ndoa imara zinazolisha famila bora. Lakini pia, jamii haiwezi kuwa bora kama hakuna familia bora.

urafiki kwenye ndoa

Rafiki, hatuwezi kuwa na waumini katika nyumba zetu za ibada kama hakuna ndoa bora. Kwahiyo, na imeandikwa ndoa iheshimiwe na watu wote lakini  watu wa kwanza  ni wanandoa wenyewe. Maisha ya ndoa ni maisha yanayodai uaminifu.

Hivyo basi, ni muhimu kama wanandoa kujifunza mbinu mpya kila siku za kuimarisha mahusiano yao ambayo ni kati ya mume na mke. Ukiwa mvivu kujifunza katika ndoa yako ni rahisi mwenza wako kukuchoka kumbe basi tunapojifunza mambo ya ndoa tunakuwa tunatengeneza mazingira mazuri ya kuimarisha ndoa zetu.

Ndoa ni agano kama tunavyojua hivyo safari ni ndefu mpaka pale kifo kitakapowatenganisha. Leo nitakufundisha mbinu bora ambayo itakuwezesha kuishi maisha bora wanayostahili kuishi wanandoa kwenye karne ya 21 na mbinu hiyo ni kuishi maisha ya urafiki kati ya mke na mume kwanini urafiki kwa sababu siku zote katika maisha rafiki ni mtu wako wa karibu hivyo unaweza kumueleza chochote kile ambacho huwezi kumwambia mtu mwingine.

Mpendwa msomaji, unakuta wanandoa wengi hawaishi huu mtindo wa urafiki na wamejenga gepu kubwa sana kati ya mume na mke. Wanandoa wasipoweza kuchukuliana kama marafiki ni rahisi sana kuchokana kwa sababu kuna wanandoa wengine hawezi kuongea hata na wanandoa wao wakiwa huru kama vile wanavyoongea na rafiki wanapokutana sehemu fulani. Kila mtu anapenda kuhisi kuthaminiwa hivyo ukimchukulia mwenzi wako kama rafiki hamwezi kuchokana.

SOMA; Epuka Tabia Hii Sana Katika Mahusiano Yako Ya Kimapenzi.

Jaribu kuishi na mke au mume wako kama rafiki hakika hamtoweza kuchokana mapema, ile hali ya kumuogopa mwenza wako itapotea na utaanza kumshirikisha vile vitu ambavyo ulikuwa unaongea na marafiki zako. Kabla ya wanandoa kuwa mke na mume waliweza kupitia hatua ya urafiki, uchumba na hatimaye ndoa. Ila hatua ya urafiki huwa inarukwa na watu wengi sana ndiyo maana watu wakiingia katika ndoa hawajuani na kila mtu anaficha makucha yake.

Mpendwa rafiki, kumbe basi watu wanapoingia katika ndoa wanakuwa wanaogopana wengine huenda ni kwa sababu ya kutojuana na kusomana katika hatua ya urafiki. Rafiki ni mtu huru kwako na unaweza kumwambia kitu ambacho huwezi kumwambia mzazi wako, ndugu nk. kama kila mwandoa akiwa huru kwa mwenza wake kama vile anavyokutana na marafiki zake basi tutaweza kuokoa ndoa nyingi sana.

Kama ukiwa kwa rafiki yako unacheka na kuongea bila aibu kwanini sasa unashindwa kuitumia mbinu hii kwa mwenza wako? Na kuongeza ladha katika ndoa yenu? Mtaendelea kuishi kwa hofu mpaka lini, mtaendelea kuogopana mpaka lini?

Hatua ya kuchukua leo, anza kutumia mbinu ya urafiki na mwenza wako kwani itakuletea ufanisi maeneo mengi. Jiachie  na jenga urafiki kwa mwenza wako na kuwa kuongea baadhi ya maneno wazi yaani bila kutumia tafsida kama unaweza kumtania rafiki yako basi mnaweza kutaniani nyie wanandoa ili kujenga ukaribu zaidi na kuishi maisha bora.

Kwahiyo, kila mwanandoa ana haki ya  kufurahia maisha, kuingia kwenye maisha ya ndoa siyo kifungo bali mntakiwa kuishi kirafiki ili muweze kuwa huru kufunguka kama vile ukiwa na marafiki zako. Rafiki ni mtu wa karibu kwako hivyo mfanye mke au mume wako kuwa rafiki yako.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.