Ukishagundua udhaifu wako, hasa kwenye muda na fedha ambapo wengi tuna changamoto kubwa, unahitaji kuwa na mbinu ambao inazuia ule udhaifu wako usiwe kikwazo.
Kwa mfano, unapokuwa na muda ambao hujaupangilia, lazima muda huo utapotea, na hutajua umepoteaje kwa sababu hukuwa umepangilia muda huo. Kwanza hutajua hata kama umepotea, kwa sababu hukuwa una mpango wowote juu ya muda huo.
Utakuja kugundua baadaye kwamba muda ulishapotea, wakati ambapo unaangalia umefanya nini na huoni ulichofanya.
Njia bora ya kuhakikisha muda wako haupotei, ni kuhakikisha hakuna muda unaouacha wazi. Pangilia siku yako nzima, pangilia kila saa yako na kila dakika. Hata kama ni muda wa kupumzika, pangilia na andika ni muda utakaopumzika.

Usiache muda wowote wazi, kwa sababu hutajua muda huo umeenda wapi, lakini ukiupangilia, utaona muda unaenda wapi na kipi hukukamilisha na kuweza kuchukua hatua haraka.
Mwisho wa siku, utaweza kuangalia ulipanga kufanya nini, na umefanya nini na kuweza kuona wapi ambapo unabaki nyuma.
SOMA; UKURASA WA 1008; Maisha Ni Mlolongo Wa Miradi…
Hili pia ni muhimu kwenye fedha, ukiwa na fedha ambayo haina mpangilio, utashangaa kuona fedha zinapotea, fedha zinatumika na hujui zimetumikaje. Unahitaji kuwa na mpangilio wa kila fedha uliyonayo, na kama nidhamu yako ni ndogo, basi tembea na ile fedha inayotosha mipango uliyonayo pekee. Usiwe na fedha kwa sababu tu unataka kuwa nayo, utajikuta umeshawishika na kuitumia kwa jambo lisilo muhimu.
Kisichopangiliwa, kisichofuatiliwa na kisichopimwa huwa kinapotea. Usipoteze muda wala fedha zako kwa kushindwa kupangilia na kufuatilia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog