Hakuna kitu chenye changamoto kwa watu wengi kama kufanya maamuzi ambayo ni magumu. Inakuwa ni changamoto kwa sababu maamuzi yanapokuwa magumu, yanatutaka tuwe na taarifa nyingi, tutafiti na kuchunguza kwa kina ili kuweza kufikia maamuzi sahihi.

Sasa hilo ni zoezi gumu, zoezi ambalo linasumbua akili na kuhitaji kazi. Hapa ndipo wengi hushindwa kuweka kazi inayohitajika, na kuchagua kufanya vitu ambavyo ni rahisi.

Na kitu rahisi kabisa kufanya, ni kuangalia wengine huwa wanafanya nini kwenye hali kama hiyo, na mtu anafanya.

Hii ni njia mbaya sana ya kufanya maamuzi muhimu kwenye maisha, ni njia ambayo inatengeneza changamoto zaidi ya kutatua, pia ni njia ambayo haileti majibu ya uhakika.

Hata kama watu wawili wanapitia changamoto moja, suluhisho moja haliwezi kuwafaa wote kwa usawa. Kila mtu kuna namna suluhisho hilo linapaswa kufanyiwa kazi ili kupata matokeo mazuri.

siyo ajali

Hapa nakwenda kukushirikisha njia za kuepuka kufanya maamuzi magumu kwa kufuata vitu rahisi.

Kwanza kabisa kuwa na msingi wa maisha yako, msingi ambao unauishi mara zote. Msingi huu utakuonesha kipi cha kufanya na kipi siyo cha kufanya kwa kila hali unayopitia.

SOMA; UKURASA WA 1006; Kutaka Kupata Na Kuepuka Kupoteza…

Pili kila wakati jiulize ni jambo lipi sahihi kufanya, jiulize ukweli ni upi na nazoea ni yapi. Mara zote kaa upande wa ukweli, na utaepuka kukosea au kuchukua hatua ambazo siyo sahihi.

Tatu usiwe na haraka, hata kama unaona maamuzi unayopaswa kufanya ni ya haraka kiasi gani, usiyafanye kwa haraka. Kadiri unavyokazana kufanya maamuzi kwa haraka, ndivyo unavyoingia kufanya vitu rahisi. Hakuna kitu ambacho hakiwezi kusubiri, na kama hakiwezi, basi pia hakitakuwa bora kabisa kwako.

Mwisho, kuwa tayari kukosea na kubadilika pale unapogundua umekosea. Usikazane kuendelea na kitu ambacho tayari umeshakosea. Endelea kuboresha zaidi, na endelea kuweka juhudi kuhakikisha unapata matokeo bora kabisa.

Maamuzi muhimu na makubwa hayapaswi kufanya kwa kukimbilia vitu rahisi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog