Reject your sense of injury and the injury itself disappears. – Marcus Aurelius
NI siku nyingine nzuri sana rafiki yangu, siku mpya ya sisi kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio, ambao unatuwezesha kuwa na maisha bora ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA. Kupitia msingi huu, tuna uhakika wa kuishi maisha ya mafanikio.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu HAKUNA ANAYEKUUMIZA, UNAJIUMIZA…
Karibu kila mtu ana hadithi ya mtu fulani ambaye amemuumiza au kuwahi kumuumiza.
Watu wengi wana watu ambao wanasema wasingekuwa wao basi maisha yao yasingekuwa na changamoto ambazo yanayo kwa sasa.
Hebu fikiri kwa kina hilo, kwa mfano ukasahau kabisa hadithi ya watu wote ambao wamewahi kukufanyia mabaya au kukutesa, je bado utasema umeumizwa?
Ninachouliza ni je kama leo ulipoamka ungekuwa umesahau kila kitu kuhusu watu waliokufanyia mambo ambayo hukitegemea, je maumivu yangetoka wapi?
Unaona rafiki, jinsi ambavyo maumivu ni matokeo ya hadithi tunazotengeneza wenyewe na kuziishi. Tukiweza kuondokana na hadithi hizi, hakuna maumivu.
Kama utasahau, na kuachana na kila ulilopitia, hutakaa na kuanza kusema umeumizwa au umeteswa.
Utaendelea kuyaishi maisha yako, ambayo umechagua kuyaishi.
Kiuhalisia tumekuwa tunajitesa na kujiumiza sisi wenyewe, pale tunapotembea na hadithi ambazo zimebeba yake tunayoamini na maumivu ambavyo wengine wametusababishia.
Mtu anayekuumiza au kukutesa, anaweza kufanya hivyo mara moja tu au mara chache, lakini wewe utaendelea kujiumiza na hadithi kwa muda mrefu.
Tuache kujiumiza, tuishi maisha yetu sasa, kwa pale tulipo.
Siku ya leo, ikawe nafasi bora ya kuweka pembeni maumivu na mateso yote uliyowahi kupitia kwenye maisha yako.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa