Kila mtu anaweza kuwa adui mzuri tu kwa mtu yeyote. Na ninaposema adui mzuri, simaanishi adui ambaye ana roho nzuri, bali namaanisha adui hasa. Lakini ni wachache sana ambao wanaweza kuwa marafiki wazuri kwa wengine.
Hii ni kwa sababu uadui hauhitaji kazi, ni mtu tu aamue kumpinga au kugombana na mwingine kwa jambo lolote ambalo kwa upande wake hakubaliani nalo, au halipendi, au siyo sahihi.
Urafiki unahitaji kazi, kazi kubwa. Unahitaji uvumilivu, wa kuweza kuyakubali mapungufu ya mwingine, na kumsaidia pale anapokwama. Urafiki ni mgumu pale unapohitajika kumtetea mtu licha ya kuwa amekosea au amefanya mambo mabaya.

Hivyo, usiogope wala kuwachukia wale wanaojenga uadui na wewe, ndiyo kitu rahisi kwao kufanya. Pia hawana uwezo wa kuweka kazi inayohitajika ili kujenga urafiki.
Pia wathamini sana wale wanaojenga urafiki na wewe, yapo mengi kuhusu wewe ambaye wanayavumilia na kuyapokea japo hawakubaliani nayo. Na wewe unapaswa kufanya hivyo kwao, kuyapokea yale ambayo huenda hukubaliani nayo, na kushirikiana kwa yale mnayoendana.
SOMA; MAHUSIANO YA KIJAMII – Namna ya kwenda na wengine.
Mwisho kabisa, adui mbaya ni yule ambaye alikuwa rafiki, kwa sababu huyu anakuwa alishapata nafasi ya kukujua wewe kwa undani zaidi. Hivyo unahitaji umakini pale mnapofikia hatua ya kutokuelewana baina yako na rafiki yako. Kazaneni kwa pamoja kutengeneza mahusiano yenu, na kama yatashindikana basi kila mmoja amheshimu mwenzake na aendelee na maisha yake.
Kumbuka, ni rahisi kujenga uadui, ni vigumu kujenga urafiki. Unapopata fursa ya kujenga urafiki na wengine, itumie vizuri kwa manufaa yenu wote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog