Uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo unaoendelea kufanyika hapa nchini unakwenda kuibadili nchi yetu katika hali ya mwonekano mpya wa zama za leo. Juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na watu ambao wameamua kwa dhati kuwa wawekezaji na wafanyabiashara katika kufikia ndoto zao za kimafanikio, hakika wamekuwa chachu ya maendeleo ya miji na vijiji kupitia huduma mbalimbali wanazotoa kwenye jamii zetu. Maendeleo ya uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo ni matokeo chanya ya mabadiliko ya kifikra kuelekea kwenye hatua mbalimbali za kimafanikio ya mtu binafsi na nchi kwa ujumla. Jamii yoyote iliyoendelea ilizingatia sana matumizi bora ya rasilimali ardhi katika kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo, ufugaji, afya, usafirishaji, elimu na miundombinu. Pamoja na juhudi zote hizo zinazofanywa na baadhi ya watu sehemu mbalimbali hapa nchini, lakini idadi yao bado ni ndogo sana ukilinganisha na rasilimali ardhi iliyopo. Ni muhimu sana ukaanza kujitathmini sasa kuhusu mchango wako wa maendeleo ndani ya jamii yako kama umeleta mabadiliko yoyote kwenye kila hatua kuelekea kwenye kufikia malengo yako.

majengo 36

Leo hii kuna idadi kubwa ya watu ambao bado wanasita sana kuchukua hatua juu ya maisha yao, kila siku mpya inapoingia swali lao huwa ni hilohilo tu, “wawekeze kwenye jambo gani”.  Pamoja na juhudi zote tunazofanya kukupa elimu na hamasa ya wewe kuanza kufanya hicho unachoamini, kwa kidogo ulichonacho, kwa ujuzi na nguvu ulizonazo lakini huchukui hatua yoyote, kwa sasa sina neno jipya kwako zaidi ya kukupa pole. Leo nitazungumzia baadhi ya mambo ambayo huathiri maendeleo katika uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo. Haya ni mambo ambayo huweza kuchochea au kudidimiza uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo.

Hali Ya Uchumi

Mabadiliko yoyote ya hali ya uchumi huwa na athari za haraka kwa wale ambao wapo kwenye hatua mbalimbali za uwekezaji wa ardhi na majengo tofauti na wale ambao wameshawekeza kwa muda mrefu. Hali ya ukuaji wa uchumi inapokuwa nzuri huchochea kwa haraka maendeleo ya matumizi bora ya ardhi na majengo, vivyo hivyo hali ya ukuaji wa uchumi inapokuwa sio nzuri huwa ni kikwazo kwa maendeleo mapya kwenye uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo.

Hali ya uchumi inapokuwa nzuri huchochea watu kujiwekea akiba na hatimaye kuwa wezesha kufanya uwekezaji kwa haraka ambao utawaletea faida na kuwafanya kuwa huru kifedha. Hali ya uchumi inapokuwa sio nzuri athari zake huonekana haraka kwenye majengo ya kibiashara tofauti na majengo yenye matumizi mengine. Hali ya uchumi inapokuwa nzuri huchochea maendeleo ya sekta nyingine ambazo huhitaji rasilimali ardhi na majengo kuwa bora na imara.

SOMA; Zifahamu Faida Pekee Za Uwekezaji Wa Ardhi Na Majengo Ambazo Ni Tofauti Na Uwekezaji Mwingine.

Nguvu Za Taasisi Za Fedha

Uwepo wa taasisi nyingi za fedha ni kichocheo kikubwa kwa mzunguko wa fedha kwenye maeneo tofauti katika kukuza uchumi. Taasisi za fedha huwa ni chachu kwenye maendeleo ya uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo endapo taasisi hizo zitatoa mikopo ya riba nafuu kwa watu. Kuwa na taasisi za fedha nyingi na zenye nguvu kwenye kuchochea wawekezaji kwa masharti nafuu na rafiki kwa wafanyabiashara, hali hii huwawezesha wawekezaji kutimiza malengo yao binafsi na jamii kwa ujumla. Ni muhimu sana kwa taasisi za fedha kuwa sehemu ya mafanikio ya wateja wake, badala ya kuwa wanyonyaji tu. Kuwa na taasisi za fedha ambazo zinatoa mikopo kwa riba kubwa, masharti lukuki na kutoweka vipaumbele kwenye uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo, hali hii itapunguza hamasa na kufifisha maendeleo kwenye jamii husika.

Ukuaji Wa Idadi Ya Watu

Tunafanya maendeleo kwa sababu ya watu, kwa kuwa maendeleo ni kwa ajili ya watu. Ukuaji mzuri wa idadi ya watu kwenye maeneo tofauti huchochea uhitaji mkubwa wa huduma mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Huduma zote hizo huratibiwa na kufanyika kwenye matumizi rasmi ya ardhi na majengo, maeneo yenye idadi kubwa ya mzunguko wa watu huchochea uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo tofauti na maeneo yenye idadi ndogo ya mzunguko wa watu. Ni muhimu sana kufanya tathimini kabla ya kufanya uwekezaji wako kwa kuangalia vigezo mbalimbali ambavyo huwa ni vichocheo vya ongezeko kubwa la idadi ya watu watakao hitaji huduma mbalimbali. Jukumu lako wewe ni kuangalia mapungufu ya wengine na kuwekeza wazo lako jipya ambalo ni tofauti na wengine.

Athari Za Sera Na Sheria

Sheria na sera mbalimbali zinazoratibu mambo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa zina athari kubwa sana kwenye maisha halisi ya jamii hiyo. Sheria na sera ambazo ni bora na zinazoendana na wakati huwa ni kichocheo kikubwa kwenye maendeleo ya watu binafsi na jamii kwa ujumla. Sheria na sera ambazo sio rafiki na haziendani na wakati kwenye jamii husika huwa na matokeo hasi ambayo hudidimiza maendeleo na hufifisha hamasa ya kufanya uwekezaji wowote ikiwemo wa ardhi na majengo.

Sheria na sera bora ni zile ambazo zitamuwezesha kila mtu kufikia malengo yake kwa haraka na ufanisi uliokusudiwa, hivyo ni muhimu sana kujijengea tabia ya kupenda kujifunza, kudadisi na kuhoji kwa uhuru na uwazi sera na sheria mbalimbali zilizopo ili ziwe zenye manufaa kwa maendeleo badala ya kuwa kikwazo ndani ya jamii. Ni wajibu wetu sote kushiriki na kutoa maoni mbalimbali badala ya kusubiri wengine waamue juu ya utaratibu na mfumo wa maisha yetu. Kuwepo kwa ruzuku kwenye vifaa na malighafi za ujenzi kutachochea kwa haraka uwekezaji wa ardhi na majengo tofauti na ikiwa hakutakuwa na ruzuku, hayo ni mfano wa matokeo ya sera.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Pale Unapohitaji Mkopo Kwa Ajili Ya Ujenzi Wa Nyumba Ya Ndoto Yako.

Hali Ya Usalama Na Amani

Hali nzuri ya usalama na amani kwenye jamii yoyote hutoa fursa ya kufanyika kwa shughuli zozote za kimaendeleo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo tofauti na jamii ambayo usalama wake ni wa mashaka. Jamii inayojali usalama wa raia na mali zao hutengeneza jamii huru na huchochea hamasa ya kufanyika kwa biashara na uwekezaji wa aina mbalimbali ikiwemo wa ardhi na majengo. Pamoja na kuwepo hali nzuri ya usalama kwenye jamii pia hali ya amani kwa mtu mmoja mmoja inapaswa kutiliwa mkazo na kutopuuzwa kwa namna yoyote.

Hali bora ya amani ni matunda ya haki, na usalama ni matokeo ya kuwepo kwa haki na amani kwa mtu mmoja mmoja.  Ni vigumu sana kufanyika uwekezaji wa ardhi na majengo kwenye jamii isiyo na usalama na amani. Tuweke juhudi kubwa katika kujenga na kuyalinda mazingira bora ya uwekezaji kwa kuhakikisha kunakuwepo na hali bora ya usalama na amani. Mafanikio ya kweli kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo ni wewe kuwa na amani na furaha wakati wote wa maisha yako.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com