Maisha bora ni kitu ambacho kila mtu anaweza kuwa na maana yake. Lakini maana nyingi haziendani na ule ubora wa maisha, ambao yeyote akiangalia anasema haya maisha ni bora.

Wengi wakisikia maisha bora basi cha kwanza kuangalia ni mali na fedha. Masikini na wale ambao ndiyo wanatafuta mali na fedha, wanaweza kuwa sahihi kwenye hilo, mpaka pale wanapozipata fedha ndiyo wanagundua kuna zaidi ya fedha.

maisha yenye maana

Vipo vitu vitatu ambavyo vinapima ubora wa maisha, vitu ambavyo kama ukivifanyia kazi, maisha yako hayatabaki hapo yalipo sasa, lazima yatapiga hatua na wengine wataona wazi. Na siyo tu wengine, bali wewe mwenyewe utaridhishwa na maisha yako.

Moja; kiasi gani unajifunza.

Dunia hii ina mambo mengi, changamoto ni nyingi na mambo mapya mengi yanakuja. Ni kiasi gani unajifunza inahusika sana kwenye ubora wa maisha yako. Wale ambao wanajifunza kila siku na wanatumia yale waliyojifunza, hawabaki pale walipo. Wanaziona fursa za kupiga hatua na wanafanya kwa ubora zaidi.

Lazima uwe mtu wa kujifunza, kupitia kila hali na kupitia kila mtu kama kweli unataka kuwa na maisha bora kwako na wale wanaokuzunguka.

Mbili; changamoto kiasi gani unapitia.

Najua unatamani kila changamoto unayopitia iondoke kabisa, ili uweze kuwa na maisha unayotaka wewe mwenyewe. Lakini kama ukikosa changamoto kabisa, maisha yatakuwa hovyo kuliko unavyoyaona sasa ukiwa na changamoto. Hebu fikiria kama ungekuwa siku nzima huna cha kufanya wala kinachokusumbua. Wewe ni kula, kupumzika na kulala. Maisha yangekuwa hovyo sana.

Kadiri unavyokutana na changamoto nyingi na kubwa, ndivyo maisha yako yanavyokuwa bora. usizikimbie changamoto, badala yake zikaribishe na zitatue ili uwe bora zaidi.

SOMA; UKURASA WA 867; Kabla Fedha Haijaanza Kukufanyia Kazi….

Tatu; mchango unaotoa kwa wengine.

Hichi ndiyo kikubwa zaidi kwenye maisha bora na yenye maana. Je una mchango gani kwa wengine? Je kipi unachotoa kwa wengine, ambacho kinawafanya kuwa bora zaidi?

Lazima uwe na mchango kwa wengine, kupitia maisha yako na kazi au biashara unayofanya. Isiwe tu unachoangalia ni fedha, bali unaangalia wengine wananufaikaje kupitia wewe. hili linafanya maisha yako kuwa ya maana na bora.

Jifunze kila siku, pokea na tatua changamoto, kuwa na mchango kwenye maisha ya wengine, fanya hayo kila siku na maisha yako yatakuwa bora sana. japo hakuna palipotajwa fedha hapo, lakini ukifanya hayo matatu, fedha zitakutafuta wewe, badala ya wewe kuzitafuta.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog