Habari za leo rafiki yangu?

Kila zama zina ustaarabu wake, ambao umekuwa unabadilika kulingana na kubadilika kwa mazingira, teknolojia na hata maendeleo mbalimbali. Pamoja na mabadiliko makubwa ambayo yamekuwa yanatokea na kubadili mambo mengi, bado watu wamekuwa wakiendelea na mambo ya zamani. Au wasijue hatua zipi za kuchukua kwa wakati ambapo wapo kwenye hali fulani. Na mbaya zaidi, watu wanaweza kuwa wanafanya kwa sababu kila mtu anafanya, wasijue maana ya wao kufanya.

Leo napenda tukumbushane ustaarabu wa zama hizi, kwa sababu kama kuna kitu kimoja ambacho watu wengi wanakikosa, ni ustaarabu. Jamii ambayo haijastaarabika ni jamii ambayo haiwezi kufanikiwa. Hivyo mafanikio yako binafsi, yanaanzia kwenye ustaarabu wako.

Angalia kwenye haya tutakayojifunza hapa, yapi umekuwa hufanyi ka usahihi na rekebisha. Au angalia yale ambayo unayafanya lakini siyo kwa kiwango kizuri na ongeza kiwango.

Vitabu

Ustaarabu muhimu kwenye zama hizi za taarifa na maendeleo ya sayansi na teknolojia;

  1. Unapokuwa na tatizo, au kukutana na changamoto kubwa, kwanza kaa chini na itafakari kwa kina. Ielewe changamoto hiyo, jua nini kimeisababisha na wewe mchago wako ni upi kwenye changamoto hiyo. Usipate changamoto na kukimbilia kuweka kwenye mitandao ya kijamii, au kuwaeleza wengine kabla wewe mwenyewe hujaielewa. Usikimbilie kuwarushia wengine lawama na kuona wewe huna tatizo. Kuna namna umechangia kila kinachotokea kwenye maisha yako, jua na ujirekebishe ili usirudie tena kwenye hali kama hiyo.
  2. Unapoahidi kitu timiza, kama huna uhakika usiahidi. Kuna vitu vidogo ambavyo vinawaangusha watu lakini wamekuwa hawajui. Moja ya vitu hivyo ni kutoa ahadi ambazo huwezi kutekeleza. Unapoahidi kitu halafu hutekelezi, watu wanajifunza kutokukuamini. Wanakuona wewe kama mtu ambaye huwezi kutegemewa, hivyo wakati mwingine ukiwaahidi, hawatakuchukulia kwa uzito. Wengine hawatataka kabisa kujihusisha na wewe ukishaanza kuonesha tabia za kukosa uaminifu. Usitake kuahidi kitu ili kuwaridhisha watu, ahidi kile ambacho unaweza kutekeleza na kama huwezi usiahidi, itakuharibia zaidi.
  3. Jifunze kukaa kimya na kutokuwa na maoni kwenye mambo mengi. Tunaishi kwenye dunia ambayo kila mtu ana maoni kwenye kila kitu. Mtu anaweza kuwa na maoni kwa kitu cha kusikia, ambacho hakijui wala hajakiona. Kwa kuwa tu amesikia watu wanatoa maoni yao, na yeye anakuwa na maoni yake. Huhitaji kuwa na maoni kwenye kila jambo, wala hutakufa kwa kuruhusu baadhi ya mambo yapite huku wewe ukiwa kimya. Jifunze kukaa kimya, kutokusema kila kitu na hata ukiulizwa, kuwa tayari kusema hujui au huna maoni. Wanasema mpumbavu akikaa kimya, anaweza kufikiriwa ni mtu mwerevu. Na hakuna ambaye amewahi kuingia kwenye ugomvi kwa kukaa kimya. Wewe siyo mpumbavu, lakini kukaa kwako kimya kutakuongezea heshima, kwenye mambo mengi.
  4. Jifunze kusema kwa matendo kuliko maneno. Tukiwa hapo hapo kwenye maneno na maoni, kuna changamoto kubwa ya kila mtu kusema lakini wachache sana kuwa wafanyaji. Watu wamekuwa wakiongea sana, lakini utendaji mchache. Usibishane na watu kwamba unaweza kufanya, fanya waone. Usianze kushauri kipi kingefanyika kingekuwa bora, kifanye. Na usianze kuwaambia mtu bora anapaswa kuishije, ishi.
  5. Matumizi na NDIYO NA HAPANA. Haya ni maneno yatakayokujenga au kukubomoa. Wengi wamekuwa wakisema ndiyo kwenye mambo ambayo wangefurahi kusema hapana, ila wanaogopa kutumia neno hapana. Wanasema ndio lakini hawatekelezi, na hili linawaharibia sifa zao. Sema ndiyo na imaanishe kweli, fanya kweli. Kama huwezi hivyo sema tu hapana, hata kama watu watachukia, watakuheshimu. Tumia ndiyo na hapana kwa uangalifu, ili usije kujiweka kwenye hali ambayo ni ngumu kwako.
  6. Kamwe usitumie zaidi ya kipato chako. Kipato chako ni laki moja, matumizi elfu tisini na tisa, wewe ni mjanja, upo pazuri. Kipato chako ni shilingi laki moja, matumizi laki moja na elfu kumi, wewe ni mpumbavu na unaelekea shimoni. Kwa nini tofauti ya shilingi elfu moja ikufanye mjanja au mpumbavu? Kwa sababu matumizi yakishazidi mapato, huwezi kupiga hatua kamwe kwenye maisha yako. Haijalishi kipato chako ni kiasi gani, ukiruhusu matumizi yazidi kipato, unapotea. Ndiyo, lala njaa, teseka lakini siyo matumizi kuzidi mapato.
  7. Popote ulipo, hakikisha umebebea kitabu. Ndiyo namaanisha kitabu halisi, najua unaweza kuwa na vitabu kwenye simu na maeneo mengine, lakini beba kitabu, tembea na kitabu na dakika chache unazopata, fungua kurasa na uzisome. Njia bora kabisa ya kujifunza bado ni kupitia usomaji wa vitabu, na kubeba kitabu halisi kunaonesha ni namna gani upo makini na kujifunza. Usikibebe kitabu tu, kisome pia. Ukishakisoma, kirudie tena na tena. Soma angalau kitabu kimoja kila mwezi, ukiweza viwili kwa mwezi, ukiweka kimoja kila wiki, au viwili, na kama upo vizuri, soma kitabu kimoja kila siku. Maarifa ya kitabu yatakusaidia sana.
  8. Mtu akikutukana usimjibu, achana naye. Mtu akikusema vibaya usimseme vibaya, achana naye. Ukimtukana aliyekutukana, au kumsema vibaya aliyekusema vibaya, unajitofautishaje naye? Kama umepita mahali mbwa akakubwekea, je na wewe unambwekea? Hivyo ndivyo ilivyo kwa watu pia. Wapo wenye matatizo yao wanataka na wewe uwe nayo, waepuke na achana nao. Matatizo yao yanawatosha, waachie wao.
  9. Kama una wasiwasi juu ya ukweli au uhalisia wa kitu, basi upo sahihi. Kwa mfano mtu kakuambia kuna fursa kubwa, kwamba ukiweka shilingi elfu kumi mahali, utapata laki moja, ndani ya muda mfupi. Mara moja utapata wasiwasi, inawezekanaje hiyo? Wasiwasi huo ni kweli, kwamba elfu kumi kuzaa laki moja kwa haraka, tena bila ya wewe kufanya kazi, haiwezekani. Hivyo usipuuzie wasiwasi wako, hata kama watu wanakuambia unaikosa fursa. Lakini pia usiishie kwenye wasiwasi huo tu, badala yake jipe muda wa kujifunza na kufuatilia, utajua na kuona ukweli uko wapi. Muhimu ni usikimbilie kuchukua hatua pale unapokuwana wasiwasi. Wanasema wasiwasi ni akili.
  10. Hichi ni kitu muhimu mno. Hakuna anayeweza kutengeneza muda zaidi. Lakini kila mtu anakazana kupoteza muda wake, kama vile upo mwingi unaokuja. Kwenye kila jambo unalofanya, jipe sekunde chache za kujibu swali hili; JE HICHI NINACHIFANYA SASA NDIYO MATUMIZI BORA KABISA YA MUDA WANGU KWA SASA? Kama jibu ni ndiyo endelea kufanya. Kama jibu ni hapana, acha mara moja na fanya kile ambacho ni muhimu. Zaidi ya nusu ya mambo unayofanya na muda wako sasa siyo muhimu sana kwako, yajue na yaache mara moja.

Haya ni mambo kumi ambayo nimependa kukushirikisha wewe rafiki yangu leo. Mengi nimekuwa nakushirikisha mara kwa mara, lakini hapa nimeyasisitiza zaidi.

Muhimu sana ni ukazane kuwa bora zaidi, ukazane kufanya yale ambayo ni uhimu na uyafanye maisha yako kuwa na maana kwako na kwa wengine pia.

Karibu kwenye program ya kusoma KURASA KUMI ZA KITABU KILA SIKU, program itakayokuwezesha kusoma vitabu hata kama huna muda kabisa. tembelea www.amkamtanzania.com/kurasa kupata maelezo ya jinsi ya kujiunga na program hii muhimu sana ya usomaji wa vitabu.

MIMI NI MSHINDI

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog