Kila mtu anayetaka kuingia kwenye biashara, huwaangalia wafanyabiashara wakubwa ambao wamepata mafanikio makubwa kibiashara.
Watu wanapowaangalia wafanyabiashara hawa, huwa wanakwama kuanza kwa sababu hawaoni ni namna gani wanavyoweza kuanzisha biashara inayoweza kuwa kubwa kama za wale wanaowaangalia.
Wengi husubiri mpaka wapate wazo ambalo ni kubwa na linaloweza kuzalisha biashara kubwa kabisa.
Lakini tukirudi kwa wafanyabiashara hao tunaowaona wakubwa leo, hawakuanza na biashara hizi kubwa. Wengi walianza na biashara ndogo, walianza na wazo ambalo walilifanyia kazi na likakua zaidi.

Hii inatuonesha kwamba, mwanzo wa biashara yoyote ile, hauhitaji kuwa mkubwa sana, hauhitaji kuwa wa kipekee ambao haujawahi kuwepo.
Badala yake mtu anahitaji kuwa na wazo na hatua anazoweza kuchukua katika kuhakikisha wazo hilo linafanya kazi.
Kwa wale ambao hawajaingia kwenye biashara na wanasubiri wakiamini bado hawajapata wazo bora, ambacho nawaambia ni kwamba wanajichelewesha. Hakuna wakati watapata wazo bora na kubwa kabisa. Wanahitaji kuanza na wazo ambalo wanaweza kulifanyia kazi, lenye hatua za kuchukua na kuweza kuongeza thamani kwa wengine.
SOMA; BIASHARA LEO; Ni hatua zipi zitakazofuata kwenye biashara yako?
Kama upo kwenye biashara na unaona biashara yako ni ndogo, haiwezi kukuletea mafanikio makubwa pia unajidanganya. Au hujaangalia vizuri. Kila biashara unayofanya, ina fursa kubwa ndani yake ya kukua zaidi na kukuletea mafanikio makubwa. Unachohitaji ni kupanga hatua za ukuaji wa biashara yako, kuboresha zaidi na kila wakati kuangalia ni thamani ipi unaweza kutoa zaidi.
Wazo unaloingia nalo kwenye biashara halipaswi kuwa ndiyo wazo utaenda nalo milele. Utabadilika kadiri muda unavyokwenda na soko linavyotaka. Hivyo ingia kwenye biashara na kazana na kitu kimoja, kutoa thamani. Mengine yatakaa sawa ukishakuwa mtu wa kutoa thamani kwa wateja wako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog