Where a man can live, he can also live well. – Marcus Aurelius

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KAMA UNAISHI, UNAWEZA KUISHI VIZURI….
Kama upo hai, haijalishi maisha yako ni magumu kiasi gani, au upo kwenye mazingira magumu kiasi gani, unaweza kuishi maisha mazuri.
Hili ni swala la kuamua ni aina ipi ya maisha unayoitaka na kuanza kuyaishi.

Wengi wanaishi maisha ambayo siyo bora kwao, lakini wanaona hawana la kufanya. Wanaona hakuna wanachoweza kufanya ili kuondoka pale walipo.
Na hapo ndipo wengi wanapojikwamisha na kukubali maisha ambayo siyo waliyokuwa wakiyataka.

Kama upo hai, unaweza kufanya kitu kuhakikisha maisha yako yanakuwa bora zaidi.
Unaweza kuchukua hatua leo, ambayo kesho itafanya uwe umepiga hatua zaidi.

Usikubaliane tu na kila hali kwa sababu unafikiri hakuna unachoweza kufanya. Badala yake jua kipi unachotaka na na kifanyie kazi ili kukipata.
Wewe siyo mti kwamba huwezi kutoka popote ulipo sasa, hata mti mambo yakiwa magumu unatuma mizizi yake kwenda mbali zaidi, au unazalisha mbegu ambazo zitaenda mbali zaidi.

Chagua maisha bora kwako, jua kipi kitakufikisha kwenye maisha bora kisha anza kuchukua hatua kuhakikisha unakuwa na maisha bora.
Uwe na siku bora sana leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa