KITABU; How to Think Like Leonardo da Vinci / Michael J. Gelb
UKURASA; 174 – 183.
Katika ulimwengu wa sasa ambao watu wanabobea kwenye mambo machache, yaani mtu anajua zaidi na zaidi kwenye maeneo machache, Leonardo anabaki na sifa ya kubobea kwenye kila kitu.
Leonardo alikuwa msanii, amechora picha nzuri na maarufu sana tangu enzi zake mpaka sasa. Ndiye aliyechora picha maarufu ya Yesu akiwa na wanafunzi wake mara ya mwisho kabla ya kusulubiwa. Pia ndiye mchoraji wa picha ya Monalisa, picha maarufu sana duniani.
Leonardo pia alikuwa na kazi nyingi za sanaa, nyingine hakuzikamilisha.
Kwa upande wa pili Leonardo alikuwa mwanasayansi aliyegundua vitu vingi sana. Leonardo alipasua wanyama wengi na mimea mingi kujifunza kipi kilichopo ndani ya wanyama hao. Pia alijifunza na kudadisi zaidi kuhusu mwenendo wa dunia na sheria za asili.
Kilichomfanya Leonardo asiwepo kwenye orodha ya wanasayansi maarufu kama kina Newton na Galileo ni kwamba Leonardo hakuwa na muda wa kuandika yale aliyogundua. Akili yake ilikuwa na mambo mengi kiasi cha kukosa muda wa kufuatilia jambo moja mpaka mwisho.
Udadisi ulimsukuma sana Leonardo katika kujifunza mambo mbalimbali. Inasemekana aliwahi kuandaa karamu ya watu wenye ulemavu ili kuwaangalia wanavyofanya mambo yao. Imeandikwa pia kwamba amewahi kumbembeleza mtu aliyekuwa anakufa, na baada ya kifo chake akaanza kumpasua hapo hapo, akitaka kujifunza kilichopelekea kifo chake.
Leonardo pia alikuwa mwanafalsafa, mtu wa kiroho aliyeishi kwa maadili na kufundisha na hata kushauri wengine kuishi kwa maadili bora.
Kwa kifupi tunaweza kusema, Leonardo aliendeleza kila uwezo uliopo ndani ya mwanadamu.
Ni wajibu wetu pia kuendeleza uwezo uliopo ndani yetu na kuacha kujilazimisha kubobea maeneo machache. Hata kama tutabobea kwenye maeneo machache, bado tunahitaji kuwa na uelewa kwenye maeneo mengine ya maisha yetu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa