Hongera sana rafiki yangu kwa nafasi hii nzuri sana ya leo. Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye yale tuliyochagua kufanya ili tuweze kupata matokeo bora zaidi.

Karibu kwenye makala yetu ya USHAURI leo ambapo tumekuwa tukipeana ushauri wa changamoto mbalimbali tunazopitia na zinazotukwamisha kufanikiwa.

Leo tunakwenda kuangalia kuhusu watu kujali yale tunayofanya. Wapo watu wengi ambao wamekuwa wanaogopa kuchukua hatua kwa sababu wanafikiria wengine watawachukuliaje. Watu hawa wamekuwa wakijikwamisha wao wenyewe kwa kutojua kitu kimoja muhimu kuhusu watu.

Kabla hatujaangalia kipi cha kufanya ili kuondokana na hali hii, tupate maoni ya msomaji mwenzetu anayepitia changamoto hii;

Mimi moyo umekuwa ukisita sana na kuogopa watu na pia kuhisi jamii itanishangaa naomba ushauri. Bundala J M.

Kama alivyotuandikia mwenzetu Bundala, wapo watu wengi ambao wanaogopa kufanya mambo kwa sababu ya wengine. Vitu kama kuogopa kuongea mbele ya wengine na hata kuanzisha biashara, vinatokana na kuwafikiria zaidi wengine kuliko sisi wenyewe.

Wengine wanaogopa kufanya vitu kwa sababu wanaona wakishindwa basi kila mtu atajua. Wengine wanaona kwa hadhi fulani ambayo wanafikiri wengine wamewapa, wakifanya kitu fulani watajishushia hadhi yao.

Yote hayo ni kujidanganya na wakati mwingine kutafuta sababu ya kuficha uvivu au kukosa utayari kunakokuwa ndani ya mtu husika.

Katika kuondokana na hali hii, nashauri mambo haya muhimu;

  1. Jua hakuna anayejali kuhusu wewe kama unavyofikiria.

Watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba watu wengine wanajali sana mambo yao. Wanachosahau ni kwamba sifa kubwa ya binadamu ni ubinafsi, hivyo kila mtu anafikiria zaidi mambo yake binafsi kuliko mambo ya wengine. Hivyo jipe uhuru, kwamba kama wewe unavyokazana kufikiria mambo yako, ndivyo na wengine wanavyokazana kufikiria mambo yao. Usijikwamishe kwa kufikiri wengine hawana cha kufanya na wanakuangalia wewe tu.

  1. Jua kila mtu anapigana vita yake mwenyewe.

Haijalishi unawaona watu wakicheka kwa nje kiasi gani, kila mtu kuna vita anapigana. Kuna changamoto na matatizo ambayo kila mtu anapitia kwa nyakati tofauti. Hivyo wakati wowote unapomwona mtu mahali, jua kuna kitu anapambana nacho kwenye maisha yake. Kitu hicho kinachukua muda wake mwingi kuliko hata mambo ya wengine. Hivyo jipe uhuru, kwa sababu wale unaowaona wanakuangalia wewe, wanakazana na mambo yao. Na wewe anza kukazana na mambo yako.

SOMA; Tofauti Hizi Ndogo Ndizo Zinakufanya Ushindwe Au Ufanikiwe Kwenye Maisha Yako.

  1. Hata pale mtu anapotoa maoni kuhusu wewe, anakusahau baada ya muda.

Kitu kingine ambacho kimekuwa kinawakwamisha wengi, licha ya hayo mawili hapo juu kuwa sahihi ni pale mtu anapotoa maoni kuhusu kile ambacho mtu anafanya. Kwa mfano mtu unaanza biashara, halafu mtu anakuambia, huwezi, hiyo biashara itashindwa. Wengi wakishapata maoni kama hayo, hufikiri kwamba aliyetoa maoni hayo anaendelea kujali na kufuatilia kitu hicho. Kumbe mtu akishatoa maoni kama hayo, anaendelea kupambana na mambo yake. Hakuna mtu ambaye anakosa usingizi usiku kwa sababu ya mambo ya wengine, kila mtu anakuwa na yake anayoyafikiria. Hivyo hata mtu anapotoa maoni ya kukatisha tamaa, usijali kuhusu mtu yule, jali kuhusu kile unachofanya.

  1. Unayemwogopa na yeye nakuogopa pia.

Kitu kimoja ambacho wengi hawapati nafasi ya kukijua ni kwamba, wakati wewe unaogopa kufanya vitu kwa sababu ya watu wengine, wapo pia ambao wanaogopa kufanya vitu kwa sababu yako. Wakati wao anaogopa wewe utachukuliaje, wewe upo ‘bize’ kuogopa wao wanakuchukuliaje. Hii ina maana kwamba, kila mtu anamwogopa mwingine, hivyo kuchukua hatua ndiyo njia pekee ya kuvunja hali hiyo. Kuendelea kuogopa watu wanaokuogopa ni kujinyima haki ya kuchukua hatua.

  1. Anza kidogo, fanya ambacho hata ukishindwa hutaleta madhara makubwa.

Wakati mwingine hofu tunayokuwa nayo kwa wengine siyo kwa sababu ya wengine, bali kwa sababu ya kile tunachopanga kufanya. Kama tunachopanga kufanya ni kikubwa na kipya, tunakuwa na wasiwasi mkubwa, tunaona tukishindwa itakuwa changamoto kubwa. Kuondokana na hali hii, anza kidogo, chagua kupiga hatua ambayo hata kama utashindwa basi hutaleta madhara makubwa kwako na kwa wengine. Kadiri unavyoanza kidogo na kushinda, unajijengea kujiamini na kupiga hatua zaidi kwa kufanya makubwa zaidi.

Usikubali kabisa kuzika ndoto zako kwa sababu una hofu wengine wanakuchukuliaje. Kila mtu anapambana na mambo yake, hivyo na wewe pambana na mambo yako, kwa kuchukua hatua kwenye yale unayotaka kufikia kwenye maisha yako.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog