Maisha yetu ni mafupi hapa duniani, ukilinganisha na umri ambao dunia imekuwa nao, sisi tuna muda mfupi mno. Kama ukikazana sana na kufika miaka mia moja, bado hujafika hata chembe ya mabilioni ya miaka ambayo dunia inayo.

Pamoja na ufupi huu wa uwepo wetu hapa duniani, bado tunafupisha zaidi maisha yetu kwa kuhangaika na vitu ambavyo havina maana kwetu. Mfano wa vitu hivyo ni kukimbizana na vitu ambavyo mwisho wa siku vinatuangusha.

Hii ina maana kwamba, mtu unakuwa umechagua kukimbiza vitu fulani, ambavyo unaamini ukivipata utakuwa na furaha na maisha yako kuwa bora. Unaweka muda wako kuvikimbiza na kweli unavipata, lakini maisha yako hayawi bora. Maisha yanazidi kuwa hovyo na inakubidi utafute kingine cha kukimbiza tena.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Acha Kuishi Falsafa Hizi Ambazo Zinakuzuia Kuishi Maisha Bora Na Ya Furaha.

Wakati huu unaokimbizana na vitu vya aina hiyo, unakuwa huishi maisha yako, unakuwa hufurahii yale maisha unayoishi, kwa sababu vile unavyokimbiza vinakuwa havina maana kubwa, ila umejishikiza navyo kiasi kwamba ukivikosa au kuvipoteza, maisha yako yanazidi kuwa hovyo.

Kusudi langu hapa siyo kukuambia usikimbizane na vitu, badala yake ninachokuambia ni kuhakikisha chochote unachofanya, kina maana kubwa kwako zaidi tu ya kupata vile vitu unavyotafuta. Kwa sababu vingi unavyopata vinaweza kupotea, lakini maana kubwa inabaki ndani yako.

Una maisha haya tu hapa duniani, ambayo ni mafupi sana na yenye ukomo. Yatumie maisha haya kufanya kile unachotaka kweli na chenye maana kwako na siyo kukimbiza vitu ambavyo mwisho wa siku vinakuangusha kwa sababu havikupi matokeo uliyotegemea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog