Kitu kimoja ambacho tunakihitaji sana lakini tunacho kwa ukomo hapa duniani ni muda. Kuna wakati tunahitaji tupate angalau muda wa ziada, ili kuweza kukamilisha mambo yetu lakini haupatikani. Lakini kuna wakati unakuta mtu alikuwa anapoteza muda, kwa kuwa hakuwa amejua kipi muhimu kufanya na muda wake.
Leo nataka tukumbushane kitu muhimu sana, ambacho kitaokoa muda ambao watu wamekuwa wanapoteza na baadaye kuja kuujutia.
Ni kuhusu kazi na biashara ambazo tunachagua kufanya.

Kazi au biashara yoyote unayoifanya kwa sababu tu unataka kupata fedha, na huna msukumo mwingine ndani yako siyo kitu kizuri kwako kufanya. Unaweza kupata fedha hizo lakini baada ya hapo utagundua kwamba kuna kitu hakipo sawa, utaona kila ulichokuwa unafanya kilikuwa kupoteza muda, na hapo ndipo unapoanza upya kutafuta kipi ufanye.
Kazi au biashara yoyote unayofanya, ukishaona unatafuta njia za mkato na za haraka za kufanikiwa kupitia kazi au biashara hiyo, jua kabisa kwamba umeshapotea. Kwa sababu kwa asili, mambo huenda kwa majira na nyakati zake. Ukishaona unataka kulazimisha majira hayo, jua huna kile unachohitajika kuwa nacho ili kufanikiwa kwenye kitu hicho.
SOMA; UKURASA WA 985; Njia Pekee Ya Kwenda Salama Hapa Duniani…
Kazi au biashara yoyote unayofanya, kwa sababu ndiyo umeona wengine wanafanya, au ndiyo uliambiwa ni nzuri kufanya, na wewe unafanya tu kwa sababu ndiyo umekuwa unafanya, itakutumbukiza kwenye shimo kubwa la upweke na kukosa maana. Kwa sababu mwisho wa siku, kila tunachofanya, tunatafuta maana ndani yetu.
Kile unachofanya kama hakileti maana, ni bora kuacha na kufanya vitu vingine. Chochote utakachopata, ambacho hakileti maana kwako, kitakuja na mateso yake. Muda wetu ni mfupi, hatuwezi kufanya na kujaribu kila kitu. Ni muhimu tukajua kipi chenye maana kwetu na tukaweka nguvu na muda wetu katika kukifanya au kuvifanya ili maisha yetu yaweze kuwa bora wakati wote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog