Katika ushirikiano wetu na watu wengine, iwe ni kwenye kazi au biashara, tumekuwa tunapenda kuwa na mikataba ili kulinda haki na maslahi yetu. Lengo la mikataba limekuwa ni kulazimisha kila upande kutimiza wajibu wake, na kuepuka kufanya maamuzi yasiyo sahihi kwa mwingine.

Watu wamekuwa wakikazana sana kupata mkataba, wakiamini mkataba ndiyo utakaowalinda. Wengi wamekuwa wakipata mikataba katika mambo mbalimbali, lakini bado mikataba hiyo imekuwa haiwalindi. Bado wamekuwa wananyanyasika licha ya kuwa na mkataba wenye kuonesha haki na stahiki zao.

mkataba

Kwa mfano mtu anaweza kuwa na mkataba wa ajira, unaoonesha kiasi cha fedha anachopaswa kulipa, au idadi ya masaa anayopaswa kufanya kazi. Lakini analipwa tofauti au anafanyishwa kazi kwa muda mrefu zaidi, na anakuwa hana namna ya kutumia mkataba huo kupata kile ambacho anastahili.

Hata katika mahusiano, wengi wamekuwa wakiamini mkataba wa mahusiano utawalinda, kwamba wakishafunga ndoa basi wana haki na uhakika wa kupata kila wanachostahili kwenye ndoa zao. wanafunga ndoa na mambo yanakuwa magumu, changamoto zinakuwa nyingi na hata makubaliano ya ndoa yanakuwa hayana msaada. Na kadiri watu wanavyotegemea mkataba wa ndoa kama salama yao, ndiyo ndoa inavyozidi kuwa ngumu kwao.

Ninachosema ni kwamba, mkataba wowote unaoingia hautakulinda wewe, unaingia tu kwa sababu ni utaratibu, ni mazoea ambayo watu wamekuwa wakifanya kwa mambo ya aina hiyo.

SOMA; UKURASA WA 1029; Huwezi Kuukimbia Ugumu, Unaweza Kuuhamisha Kwa Muda.

Hivyo usijidanganye kwamba ukishapata mkataba basi upo salama, usalama wako uko sehemu moja tu, kuchagua watu sahihi wa kujihusisha nao. Kama ni kazi basi chagua kufanya kazi kwa mwajiri sahihi, mwajiri mwenye utu na mwenye uadilifu mkubwa. Kama ni biashara basi chagua kufanya biashara na mtu mwenye uaminifu na uadilifu wa hali ya juu, mtu ambaye yupo tayari kujitoa sana. Na inapokuja kwenye ndoa, chagua mtu ambaye ana tabia nzuri tayari, siyo mtu wa kusema tutarekebishana tabia, chagua mwenye tabia nzuri tayari na ambaye mnaweza kuvumiliana kwa zile changamoto ambazo hakuna anayezikosa.

Nirudie tena, usikazane sana na mikataba ukafikiri ndiyo usalama wako, ukiingia mkataba na mtu mwenye tabia mbaya, mkataba huo utakuwa moto zaidi. Kitakachokuokoa ni kuchagua watu sahihi, watu ambao watakuwa tayari kwa ajili yako na kukuthamini wewe kama wewe na siyo kwa sababu kuna mkataba.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog