Rafiki, vimeandikwa vitabu vingi sana kuhusu mafanikio, vingi mno.

Zimeandikwa makala nyingi mno kuhusu mafanikio, nyingi kuliko unavyoweza kusoma.

Lakini bado mafanikio yanaitwa siri. Yaani vitu ambavyo vipo wazi kwa kila mtu, vikishahusisha mafanikio basi tunaweza kuviita siri na watu wasiudhike kwa namna yoyote ile.

Kwa mfano naweza kuandika hizi ndiyo siri kuu tano za mafanikio kwenye maisha.

Halafu nikakuorodheshea kuwa na maono, kuweka malengo, kuweka juhudi kwenye kazi, kushirikiana na wengine vizuri na kujifunza kila siku.

Kipi kati ya hayo matano ndiyo umekisikia kwa mara ya kwanza leo? Lakini imekushangaza chochote kwa kuziita hizo ni siri?

Kila kinachohusisha mafanikio kimekuwa kinaitwa siri kwa sababu watu wanayapenda mafanikio lakini hawayaelewi mafanikio. Watu wanatamani sana kufanikiwa, lakini hawajapata kujifunza kwa kina kipi hasa kinachoweza kuwafikisha kwenye mafanikio.

Msingi Mkuu

Hivyo wanajaribu njia zao wenyewe, ambazo haziwaletei mafanikio. Lakini wanawaona watu wengine kama wao, ambao hawatofautiani sana, wanafanya kile wanachofanya wao, lakini wana mafanikio makubwa kuliko wao. Hapa ndipo watu wanapopata hisia kwamba huenda wale waliofanikiwa kuna kitu wanajua, ambacho wao hawajui na hivyo mtu anaposema ipo siri ya mafanikio, watu wanaamini kutakuwa na siri kweli, kwa sababu wao wamekazana sana na hawajayapata.

SOMA; NYEUSI NA NYEUPE; Hii Ndiyo Ile Hela Ya Sigara (Jinsi Unavyoweza Kuweka Akiba Kidogo Kidogo Mpaka Kufikia Utajiri).

Ukiangalia maisha watu wanayoishi sasa, na yale ambayo watu wanafanya kila siku, mafanikio yataendelea kuwa siri kwa wengi. Kwa sababu wengi hawana utayari wa kufanikiwa, wengi hawajajitoa kweli kufanikiwa. Na vinapokosekana vitu hivyo viwili, lazima mafanikio yaendelee kuwa siri kubwa kwa wengi.

Leo sikupi siri, na wala sikuambii kitu ambacho hujawahi kusikia kabisa. bali ninachokwenda kufanya hapa ni kukukumbusha yale ambayo nimekuwa nakuambia mara kwa mara kupitia mafunzo ambayo nimekuwa nayatoa. Nimeona inafaa kurudia na nitaendelea kurudia hili kwa sababu idadi ya watu wanaolipuuza inazidi kuwa kubwa kila siku.

Lipo jambo moja muhimu sana unalopaswa kulijua kuhusu mafanikio yako kwenye maisha, na kama tayari unalijua basi unahitaji kuendelea kujikumbusha kila siku ya maisha yako.

Jambo hilo ni kwamba, mafanikio yoyote unayohitaji kwenye maisha yako, yanahitaji muda wako mwingi mno. Nirudie tena kusisitiza, chochote unachohitaji kufanikiwa, kitakuchukua muda wako mwingi mno.

Nasisitiza hili kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo hili linavyozidi kusahaulika. Kwa hali ya sasa ambapo michezo ya kubashiri na kubahatisha inapamba moto, watu wanazidi kushawishika kwamba mafanikio ni kitu cha bahati tu ambayo inaweza kumwangukia yeyote.

Katika zama hizi ambazo kila siku kuna aina mpya ya fursa na uwekezaji inajitokeza, ambapo watu wanashawishika wanaweza kuweka fedha mahali na ndani ya muda mfupi ikazalisha faida kubwa sana, watu hawaelewi tena umuhimu wa muda.

Watu wengi wamekuwa wanakimbilia mambo hayo rahisi na ya muda mrefu, wanahangaika nayo lakini mwisho wa siku wanajikuta wapo pale pale, hakuna hatua yoyote ambayo wanakuwa wamepiga. Wakiwaangalia wengine ambao wamefanikiwa, wanaamini kuna kitu wanakijua ambacho wao hawakijui.

Na hata pale waliofanikiwa wanapowashirikisha kile kinachowafanya wafanikiwe, kwa kuwa kinaonekana cha kawaida, ambao hawajafanikiwa hawaamini. Wanajishawishi kwamba wanadanganywa, siri ipo lakini haitolewi.

Niendelee kukuambia rafiki yangu, hakuna siri ambayo imefichwa, wala hakuna siri mpya ambayo inakuja. Ni wewe uchague kuweka muda na juhudi zako kwenye kile ambacho unataka kukifanya, uwe mvumilivu na mwisho wa siku utafanikiwa.

Ukishaamua kile unachotaka, usianze tena kutafuta njia za mkato au kubabaika na yale ambayo wengine wanakuambia ni bora zaidi ya kile ulichochagua kufanya. Na pale watu wanapokuja kwako na kitu ambacho ni cha mkato na rahisi, kisichohitaji muda, ni vyema ukaachana nao mara  moja, wala usitake kusikiliza, jua hao wanapoteza muda wao na ukiwasikiliza utapoteza muda wako pia.

Mafanikio yoyote kwenye maisha yako, yanahitaji muda, chochote chenye thamani kinahitaji muda. Kuwa tayari kuweka muda, kazi na juhudi kubwa ili kuweza kufika kule unakotaka kufika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog