A quarrel is quickly settled when deserted by one party; there is no battle unless there be two. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UGOMVI UNAHITAJI PANDE MBILI…
Kama umewahi kujikuta kwenye ugomvi wa aina yoyote na mtu au watu wengine, basi jua ya kwamba wewe ulichangia ugomvi huo.
Hata kama makosa ni ya wengine, ukishaibuka ugomvi basi wewe pia unakuwa umechangia ugomvi huo.

Hii ni kwa sababu hakuna ugomvi wa mtu mmoja. Ugomvi unahitaji watu wawili, wakwaruzane na wajibishane vibaya.
Iwapo upande mmoja utaepuka kukwaruzana na kujibizana, ugomvi hauwezi kutokea, au hata ukitokea hauwezi kuwa mkubwa.

Hivyo rafiki, kama hutaki ugomvi, basi hatua ya kwanza ni kuacha kuchochea ugomvi.
Pale mtu au watu wengine wanapotaka kukuingiza kwenye ugomvi, jiweke pembeni kwa kuacha kushiriki moja kwa moja.
Kwa mfano kama mtu amekujibu vibaya, au amekuambia maneno mabaya, ukimjibu maneno mabaya unachochea ugomvi, lakini ukikaa kimya, hawezi kuendelea na maneno yake hayo. Kwa sababu ugomvi unakuwa hauna raha kama upande mmoja ndiyo unaofanya kila kitu.

Lakini hili halimaanishi ukubali watu wafanye chochote wanachotaka na wewe ukae tu kimya. Badala yake unahitaji njia bora ya kutatua chochote kinachotokea, lakini isihusishe ugomvi.
Unaweza kumwacha mtu kwa muda na baadaye ukamweleza ni kwa namna gani hukufurahishwa na alichosema au kufanya.

Hakuna kitu kinachopoteza muda, nguvu na hata heshima kama magomvi ya mara kwa mara.
Kataa kujihusisha na aina yoyote ya ugomvi, kuwa na njia bora ya kutatua hali yoyote ya kutokuelewana unayokutana nayo.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha