Nimewahi kusoma ujumbe mmoja wa kufundisha katika jumbe ambazo huwa zinasambazwa kwa njia ya simu. Katika ujumbe huu, muumini wa kanisa alikwenda kwa mchungaji na kumwambia hataki tena kuhudhuria ibada kwa sababu kila anapokuwa kwenye ibada anaona watu wakifanya mambo yasiyofaa. Wengi wanakuwa wanachezea simu zao, wengine wanapiga umbeya na mambo yasiyofaa.
Mchungaji alimwambia sawa, anakubaliana naye kuhusu kutokwenda tena kanisani, lakini alimwomba afanye kitu kimoja na akishakifanya basi atamruhusu asiende tena kanisani. Alimwambia wakati wa ibada, atembee na glass iliyojaa maji kutoka mwanzo mpaka mwisho wa kanisa mara mbili bila ya kumwaga hata tone moja. Muumini yule alikubali na wakati wa ibada alichukua glass yake yenye maji yaliyojaa na kutembea nayo mwanzo wa kanisa mpaka mwisho mara mbili bila kumwaga.

Baada ya ibada ya ibada alikwenda kwa mchungaji, na mchungaji akamuuliza, je ulipokuwa unatembea na glass ya maji, uliona watu wakichezea simu zao na kupiga umbeya? Muumini akajibu hapana, nilikuwa naangalia glass kwa umakini. Mchungaji akamwambia hicho ndiyo unapaswa kujua, kama ukija kanisani na kuangalia kile kilichokuleta, hutaona mapungufu ya wengine.
Hapa lipo somo kubwa sana tunaloweza kujifunza na likatusaidia kwenye safari yetu ya mafanikio. Kuna wakati watu tunapata hofu kubwa sana kwamba huenda kile tunachofanya tunakosea au tutashindwa. Pia wakati mwingine tunaweza kuona sisi tunakosea na wengine wapo sahihi zaidi. Au tukaona wengine wanakosea na sisi ndiyo tupo sahihi zaidi.
SOMA; UKURASA WA 908; Kila Mtu Anaona Kile Anachojua…
Ukweli ni kwamba, utaona hofu kama utaacha kuangalia ndoto yako kubwa kwenye maisha. Utaona wengine wapo vizuri zaidi kama utaondoa macho kwenye ndoto kubwa ya maisha yako.
Ukishaanza kuangalia mambo mengine na kuacha kuangalia ndoto yako, utaona kila kitu cha kukushawishi kwamba ndoto hiyo haikufai au siyo sahihi kwako. Ni rahisi zaidi kwako kuachana na ndoto yako kubwa kama utaacha kuiangalia na kwenda na mambo mengine.
Ndoto kubwa ya maisha yako, maono unayotaka kufikia na malengo na mipango yako vinapaswa kuwa vitu ambavyo muda wote unaviangalia. Vinapaswa kuwa kwenye akili yako muda wote, ukiamka vipo kwenye mawazo yako, unapata taswira ya kule unakokwenda. Hii inakuwa hamasa kwako na hata unapokutana na magumu au changamoto, inakuwa rahisi kwako kuzivuka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog