Habari za leo rafiki yangu?

Hongera kwa nafasi hii ya kipekee ya leo, ambapo tumepata nafasi ya kwenda kuweka juhudi zaidi kwenye yale tunayofanyia kazi kwenye maisha yetu. Kuiona siku ya leo pekee ni ushindi mkubwa kwako, itumie siku hii kupiga hatua zaidi.

Kila mmoja wetu anahitaji ushauri kwenye mambo mbalimbali ya maisha. Tunahitaji ushauri kwenye maisha yetu binafsi, kazi zetu, biashara zetu, mahusiano yetu na maeneo mengine ya maisha yetu.

Lakini watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba hawana nafasi ya kupata ushauri mzuri. Wamekuwa wakifanya mambo ambayo siyo bora kwao kwa sababu hawana watu wa kuwashauri vizuri.

Watu wanakosa watu wa kuwashauri kwa sababu wamekuwa wakichagua ni ushauri wa nani wanaweza kuuchukua na kuufanyia kazi. Ni kawaida yetu binadamu kupenda kuwasikiliza na kuchukua ushauri kutoka kwa wale ambao tayari wamefanikiwa.

Kumekuwa mpaka na utani kwamba mwenye fedha anasikilizwa zaidi hata kama ni mdogo kuliko mkubwa ambaye hana fedha. Ndiyo uhalisia wa dunia ulivyo, kwa sababu tunaamini mtu akishakuwa na fedha nyingi basi anajua mengi zaidi. Hili linaweza kuwa sahihi na pia kuwa siyo sahihi.

Dunia Inajiendesha

Ukisema usubiri mpaka upate mtu aliyefanikiwa ndiyo akushauri, utakosa ushauri kwa sababu waliofanikiwa ni wachache, na hawana muda wa kumshauri kila anayetaka kupata ushauri kutoka kwao. Wengi wa waliofanikiwa wanakazana kufanya yale wanayofanikiwa na hivyo ni vigumu kuwapata wakushauri kwenye kila unachofanyia kazi.

Pia wapo watu ambao kazi au biashara yao ni ushauri. Watu hawa wanakuwa wamejifunza na kupata uzoefu ambao wanawashirikisha wengine na wanaweza kupiga hatua. Watu hawa wanaweza kuwa wazuri sana kama wanatoa matokeo bora kwa wale wanaowashauri. Lakini hawa pia wana changamoto moja, kadiri mtu anavyotoa ushauri bora, ndivyo gharama zake zinavyokuwa kubwa. Kupata muda wa kukaa na mtu huyo anayetoa ushauri mzuri itakugharimu kiasi kikubwa sana, ambacho huenda huna.

SOMA; Sheria Tano Za Fedha Unazopaswa Kuzijua Na Kuzisimamia Kama Unataka Kuondoka Kwenye Umasikini.

Hivyo kwa kuangalia hali hizo mbili, kwamba waliofanikiwa hawana muda wa kukupa ushauri unaotaka, na wanaofanya kazi ya kutoa ushauri gharama zao ni kubwa, unaweza kuona umebaki bila ya msaada. Kwamba huna wa kukushauri na hivyo unafanya mambo kwa kubahatisha pekee.

Huo siyo ukweli, na leo nakuandikia kukuonesha fursa kubwa ya ushauri uliyonayo hapo ulipo wewe, ambayo hujaanza kuitumia. Kama ukiijua fursa hiyo na kuanza kuitumia, utanufaika sana, utaepuka makosa mengi na kuweza kujua hatua sahihi za kuchukua ili kufanikiwa.

Upo ushauri wa bure, unaokuzunguka hapo ulipo wewe, ambao unaweza kuutumia vizuri sana kwenye maisha yako.

Ushauri huo ni kupitia wazee ambao wanakuzunguka hapo ulipo wewe. kila mzee unayemuona, ambaye amekuwa hai kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita, ni ushauri bora kabisa kwako unaoweza kuutumia.

Najua unajua kwamba wazee wanaweza kukupa ushauri mzuri, lakini kitu ambacho hujui ni jinsi gani unaweza kupata ushauri huo. Kwa sababu wengi huenda kwa wazee hawa na kuanza kuwauliza ufanye nini kwa hali ambayo unapitia wewe. Na hapa wao wanafanya kile ambacho wewe unawategemea wafanye, kukueleza kitu kizuri unachoweza kufanya.

Lakini kwenye ushauri unachohitaji siyo kitu kizuri unachoweza kufanya, bali unahitaji kuondoka na hatua za kuchukua mara moja.

Hivyo ili kupata ushauri mzuri wa wazee wanaokuzunguka, waendee na swali hili; je kama ungepata nafasi ya kuwa kijana tena, ni kitu gani ungefanya tofauti?

Unamuuliza mzee kama angepata nafasi nyingine ya kuanza ujana, je mambo gani angeyafanya tofauti?

Swali hili linamfanya mzee awe mwaminifu kwake na kwako pia. Linamfanya mzee atoe majuto yake ambayo amekuwa nayo kwa muda mrefu. Swali hilo linamfanya akumbuke nafasi alizowahi kuzipoteza kwenye maisha yake, na mambo mengi aliyojifunza kupitia watu wengine katika kipindi chote cha maisha yake.

Mtu yeyote ambaye amekuwa hai kwa zaidi ya miaka 60, ameona na kujifunza mengi, hata kama hajawahi kusafiri au amekuwa kijijini. Katika miaka yote hiyo, amejaribu mambo mengi, mengine yakawa mazuri na mengine mabaya. Katika kipindi chote hicho, ameona watu wakifanya mambo ambayo yanawasaidia na ambayo yanawapoteza.

Kama ukiweza kuyapata hayo, yatakusaidia sana katika kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako. Yatakuwezesha kujua wapi pa kuzingatia na wapi pa kuepuka ili usiingie kwenye matatizo na changamoto.

SOMA; NYEUSI NA NYEUPE; Kuhusu Kufanya Kazi Kwa Nguvu Na Kufanya Kazi Kwa Akili.

Nimalizie kwa kutoa onyo kwa watu wa kizazi hichi, siyo tu vijana na watoto, bali watu wote ambao kwa sasa bado wanakazana kupiga hatua kwenye maisha. Ipo kasumba kwamba mambo yamebadilika sasa, na ushauri wa wazee umepitwa na wakati. Kwamba wazee hao wameishi kipindi ambacho hakukuwa na simu, kompyuta wala mitandao ya kijamii, hivyo chochote walichojifunza, hakina matumizi kwenye zama hizi.

Huo ni uongo na kujidanganya kwa hali ya juu. Miaka ya hivi karibuni nimebadili mfumo wangu wa kusoma vitabu, nimekuwa nasoma zaidi vitabu ambavyo vina zaidi ya miaka 500, yaani vitabu vya zamani mno. Vitabu vilivyoandikwa na wanafalsafa walioishi miaka zaidi ya 2000 iliyopita. Wanafalsafa kama Socrates, Aristotle, Seneca, Epictetus na wengine wengi. Na kikubwa ninachojifunza ni kwamba pamoja na miaka mingi kupita, mafunzo na ushauri waliokuwa wanatoa, unatufaa sana katika kipindi hichi. Tena naweza kusema ushauri wao ni muhimu zaidi katika zama hizi kuliko hata zama walizoishi wao.

Nimekuwa najifunza na kuona namna ambavyo hakuna kitu kipya hapa duniani, mambo ni yale yale ila yanakuja kwa mfumo tofauti. Kwa mfano moja ya vitabu vya mwanafalsafa Seneca kinachoitwa ON THE SHORTNESS OF LIFE, Seneca anaeleza jinsi maisha yalivyo mafupi, jinsi muda ulivyo mfupi lakini watu wanaupoteza kwa kufanya mambo yasiyo na maana kabisa. Hichi ni kitabu ambacho kimeandikwa zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita, lakini hebu angalia leo. Watu wanapoteza muda na maisha yao kwenye TV, simu, mitandao ya kijamii, habari zisizo za maana, umbeya na majungu na kufuatilia wengine. Kwa maoni yangu binafsi, hakuna kipindi ambacho watu wanaamua kupoteza muda na maisha yao kwa ujumla kama sasa.

Hivyo rafiki yangu, kaa na wazee wanaokuzunguka, na swali lako kwao ni moja, je kama ungepata nafasi ya kuanza ujana sasa, kipi ungefanya tofauti? Halafu hoji maswali mengi zaidi, omba ufafanuzi zaidi, omba mifano zaidi na utajifunza mambo mengi mno.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog