Habari za jioni ya leo rafiki yangu?
Ni imani yangu kwamba umekuwa na siku bora sana leo.
Ni matumaini yangu siku ya leo umeweza kupiga hatua na pia kujifunza zaidi kupitia yale uliyoweza kukutana nayo.
Na sina shaka kwamba leo umeishi msingi wetu wa maisha ya mafanikio ambao ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

Karibu kwenye tafakari ya jioni ya leo, ambapo nakwenda kukushirikisha ujumbe mfupi wa kukufanya utafakari na kufikiri maisha yako kwa kina na uweze kupiga hatua zaidi.
Jioni hii napenda utafakari kuhusu KUISHI WAKATI UNAWEZA…

Imekuwa ni tabia yetu wanadamu kuahirisha maisha, kuacha kuishi leo na kufikiri kwamba kesho tutakuwa tayari kuishi.
Huwa tunaona leo hatujawa tayari, kwa sababu labda kuna kitu hatujakamilisha.
Labda hatujapata kazi tunayotafuta,
Au bado tupo kwenye masomo,
Au hatujaanza biashara tunazotaka,
Au hatujafikia malengo tuliyojipangia.
Kwa chochote kile ambacho tunajiambia leo hatujaanza maisha tunajidanganya.
Tunajidanganya tunapofikiri kesho itakuwa bora zaidi kuliko leo na hivyo kuahirisha kuishi leo.
Pia tunajidanganya pale tunapofikiri kwamba maisha yetu hayana mwisho, au kama upo, siyo kesho wala siku za karibuni.

Ishi maisha wakati unaweza kuyaishi, ishi maisha yako sasa, kwa pale ulipo, kwa kile ulichonacho.
Wakati wowote kwa popote ulipo, tayari umekamilika kwa maisha.
Sehemu unayopaswa kuwa kwa sasa, hi hapo ulipo, hapo ndipo ulipo sasa, ambapo huwezi kupakimbia bali kupaishi.
Na kama unataka kupiga hatua zaidi, lazima uanzie hapo ulipo sasa, lazima uwe umeishi hapo ulipo.

Maisha yako ni sasa, ishi wakati unaweza kuyaishi.
Maisha yako ni hapo ulipo, yaishi sasa na acha kuahirisha.
Kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, lazima uishi sasa, lazima uanzie hapo ulipo.

Uwe na jioni njema rafiki yangu, ukaipangilie siku yako ya kesho vyema ili kuweza kufanya makubwa.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha