Mafanikio tunayoyatafuta kwenye maisha, yanatoka kwa watu wengine. Chochote tunachotaka kwenye maisha yetu, tunategemea kitoke kwa watu wengine.

Kadiri watu wanavyotujua na kutuamini, ndivyo inavyokuwa rahisi kwetu kupata kile ambacho tunataka kutoka kwao.

Kila Mtu

Katika hili la watu kutujua na kutuamini, yapo mambo mawili muhimu sana ya kuzingatia kwetu sisi wenyewe.

Jambo la kwanza ni unaweza kufanya nini?

Hili ni muhimu kwa sababu kitu cha kwanza watu wanachofikiria wanaposikia jina lako au kukumbuka kuhusu wewe.

Kile unachoweza kufanya na unachofanya kwa wengine, ndiyo kinabeba sifa yako kwa wengine.

Umewahi kumfanyia mtu kitu, halafu mkapotezana, lakini siku moja akakutafuta wakati ana shida ya kile ulichomfanyia? Hichi ndiyo tunazungumzia hapa.

Kujijengea sifa ya kuwa mtu wa kufanya, hivyo mtu anapokuwa na shida kwa eneo linalohusiana na wewe, anakufikiria wewe mara moja kabla hata hajapata mawazo ya watu wengine.

Zingatia kuhusu nini unafanya, siyo nini unasema unaweza kufanya. Ufanyaji unabeba sifa kubwa kuliko usemaji. Fanya vitu vitakavyokujengea sifa kwa wengine. Tatua changamoto zao, wasaidie matatizo yao na watakufikiria wewe kila unapokuwa na uhitaji.

SOMA; UKURASA WA 779; Usichukue Ushauri Kwa Mtu Wa Aina Hii…

Jambo la pili ni maisha yako yana mfano gani?

Aina ya maisha ambayo unaishi wewe binafsi, inawafanya watu wakujue na kukuamini au wakujue na kukudharau au kutokukuamini.

Maisha unayochagua kuishi, tabia ulizonazo, ni kitu cha kwanza ambacho watu wanakiona kwako. Hivyo kama utachagua kuishi maisha yaliyo nyoofu, ukawa na tabia zilizo bora, watu watakuamini na watakuwa tayari kukupa kile unachotaka.

Tabia zetu zina mchango mkubwa sana wa popote tunapofika kwenye maisha. Wapo ambao wamekuwa wanasema wana kisirani au bahati mbaya pale wanapokataliwa na wengine. Lakini ambacho hawajui ni kwamba, tabia zetu zipo wazi, hatuwezi kuzificha na kila mtu anaweza kuzisoma.

Kuwa mtu wa kufanya na julikana kwa kipi unaweza kufanya, pia ishi maisha ya mfano kwa kuwa na tabia bora sana. Haya mawili yatakuwezesha kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine na kupata kile unachotaka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog