Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza changamoto moja ya kuepuka kumshirikisha mtoto wako. Je unajua ni ipi? Karibu tujifunze.

02638-malezi

Rafiki, watoto wanapitia katika changamoto mbalimbali za kimalezi ambazo zinawafanya kuona dunia ni sehemu mbaya kwao kuishi. Wanapitia vitu ambavyo hawastahili hata kuviona kwenye maisha yao hii yote ni kutokana na wazazi, walezi au jamii husika kukosa elimu sahihi.

Utandawazi nao unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuharibu watoto uwezo wa ubunifu, watoto wanakosa ubunifu wa kujitengenezea hata michezo yake mwenyewe kwa sababu ya akili yake imeshafungwa na utandawazi kwa kulemezwa na michezo ya kisasa anayonunuliwa au kuona katika TV au Apps mbalimbali na kwenye mitandao ya kijamii.

SOMA; Kanuni Bora Ya Malezi Ya Watoto Yenye Mafanikio Makubwa

Changamoto moja ya kuepuka kumshirikisha mtoto wako ni changamoto za kimahusiano. Wazazi wanakosea sana pale wanapowashirikisha watoto wao wadogo au hOata wakubwa changamoto zao za kimahusiano wanazopitia. Ni jambo la aibu na fedhea sana kwa mtoto kusikia changamoto za kimahusiano za wazazi wake, huwa tunawapa mizigo mikubwa ambayo bado hawastahili kuibeba ni kama vile mtoto anayezaliwa leo analazimishwa kukaa na kutambaa mara moja.

Kama unachangamoto zako za kimapenzi na mwenzako usimshirikishe mtoto wako, watoto wanaanza kujazwa sumu mapema za mahusiano kabla hata hawajaingia katika wito waliouchagua hapa duniani. Tunapowashirikisha matitizo ya kimahusiano tunawapa hofu mapema ya wao kuogopa kuingia katika mahusiano ya ndoa pale wanapokuwa wamefikia hatua ya kutaka kuoa au kuolewa.

Watoto wanajazwa sumu kuwa baba ni mbaya sana au mama yako ni mbaya sana anafanya moja, mbili , tatu sisi tukiona ni vizuri kumbe tunawaharibu ndiyo maana kuna watu unawakuta hawataki kabisa kusikia kuhusu mwanamke au mwaname hii huenda ni zile sumu alizokuwa akilishwa za mahusiano alipokuwa mdogo. Kuna wazazi wengine wanajua watoto huwa hawaeleti hivyo hata wakiongea mambo yao hadharani hayana athari kumbe yanaathari kubwa sana.

Hatua ya kuchukua leo, haijalishi unapitia magumu kiasi gani lakini ni mwiko kumshirikisha mtoto au watoto wako changamoto mbalimbali unazopitia. Ukianza kumwaminisha mtoto wako  changamoto zako za kifedha na kumpa imani hasi juu ya maisha utakuwa umefanya kazi ya kumuua mwenyewe.  Mjengee mtoto imani chanya juu ya vitu vyote na siyo hasi.

SOMA; Jinsi Ya Kumfundisha Mtoto Kuvua Samaki.

Kwahiyo, ili tuweze kujenga jamii bora, tunatakiwa kwanza tujengee ndoa bora na hapo ndipo tutaweza kuzalisha familia bora. Familia ni mali ya jamii hivyo kama familia ikiwa bora jamii nayo inafaidika kwa ubora huo. Kuwa sehemu ya mabadiliko unayotaka kuyaona kwa mtoto wako na ni vizuri kujifunza juu ya malezi ya watoto.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.