Mafanikio yangekuwa rahisi, kila mtu angekuwa na mafanikio makubwa. Siyo rahisi ndiyo maana wachache sana ndiyo wenye mafanikio. Na ugumu wake unawafanya wengi waamini ipo siri ya mafanikio ambayo wao hawaijui.
Leo nataka tujadili Hapana ya mwingine na Ndiyo yako.
Chochote unachotaka kwenye maisha yako, utakipata kupitia wengine.
Lakini sasa, wengine hao hawatakupa kiurahisi kama unavyofikiri. Wengi ambao unategemea wakupe unachotaka, hawatakupa. Utakutana na hapana kwenye mengi na kwa wengi.
Na hapo ndipo ndoto za wengi zinapoishia, baada ya kuambiwa hapana na wengine, hukubaliana na hapana hiyo na kuona hakuna wanachoweza kufanya.
Wengine watasema nimehangaika sana lakini kote nashindwa.
Ili kuweza kuvuka hili na kuweza kupata unachotaka na kufanikiwa, unapaswa kujua vitu viwili muhimu. Kuna hapana ya wengine, halafu kuna ndiyo yako.

Wewe unaposema unataka kitu fulani, unapopanga kufika mahali fulani, hiyo ndiyo NDIYO yako. Hii ni ndiyo ambayo unapaswa kuifanyia kazi kwa namna yoyote ile ili uweze kuifikia. Unapohitaji kitu kutoka kwa wengine wakakuambia hapana, hiyo ni HAPANA yao.
Hapana ya wengine haipaswi kuwa na nguvu kuliko ndiyo yako. Pale utakaporuhusu hapana ya wengine iwe na uzito kuliko ndiyo yako, unakuwa umechagua kushindwa kabla hata hujaanza. Kwa sababu utakutana na HAPANA nyingi mno kwenye maisha yako.
SOMA; UKURASA WA 953; Unachokichukia, Unakipa Nguvu Ya Kuendelea Kukusumbua…
NDIYO kubwa iliyopo ndani yako ndiyo itakayokuwezesha kupiga hatua. Hata pale watu wanapokuambia huwezi au haiwezekani, ndiyo iliyopo ndani yako itasema hebu tuone itakuwaje, kisha unafanya. Pale mmoja anaposema HAPANA, NDIYO iliyopo ndani yako inasema wapo wengine wengi zaidi, hebu tuendelee kutafuta watakaotuelewa.
Usije ukajidanganya kabisa kwamba wale unaoona wamepiga hatua hawajakutana na HAPANA. Wamekutana nazo nyingi, lakini NDIYO kubwa zilizopo ndani yao zimeweza kushinda hapana hizo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog