Kuna vitu ambavyo wewe unataka kwenye maisha yako ili kufika kwenye yale maisha unayotaka. Labda ni fedha nyingi, mali, umaarufu, mahusiano bora na kadhalika.
Kuna vitu ambavyo dunia inataka ili iweze kutoa chochote ambacho kipo ndani yake. Labda ni uchapakazi, uvumilivu, ushirikiano na kutoa kile ambacho wengine wanahitaji.
Kukazana na kile unachotaka wewe pekee, inaweza kuwa ngumu sana kwako kukipata, kwa sababu hakuna chochote unachotaka ambacho kitatoka ndani yako mwenyewe.
Lakini kama utakazana na kile dunia inataka, itakuwa rahisi kwako kupata kile unachotaka, kwa sababu ukiipa dunia kile inachotaka, na yenyewe itakupa kile ambacho unataka.

Ukiweka juhudi katika kazi, dunia haitakuwa na ubishi bali kukupa wewe matunda mazuri ya kile unachotaka.
Ukiangalia changamoto na matatizo ya wengine halafu ukaweka juhudi katika kuyatatua, wao watakuwa tayari kukupa kile ambacho unataka kwenye maisha yako.
Dunia inaendeshwa kwa sheria za asili, na moja ya sheria kuu zinazoendesha dunia ni NIPE NIKUPE. Dunia inawapa wale ambao kuna kitu wanatoa, na kuwanyang’anya wale ambao hawatoi chochote badala yake wanataka tu.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Njia Ya Uhakika Ya Kuwafanya Watu Wakupe Kile Unachotaka.
Hii ndiyo sababu huwezi kuona watu wanaopenda kulalamika wakiwa wamefanikiwa, huwezi kuona wezi na mafisadi wakiwa na amani ya moyo kwa chochote walichopata. Ni kwa sababu matendo hayo yanaenda kinyume na sheria ya dunia ya NIPE NIKUPE.
Ni vizuri sana kutaka makubwa, na kujua kwa hakika ni nini unataka. Lakini ni muhimu zaidi kujua dunia inataka nini na kujua unaipaje dunia kile inachotaka. Na ninaposema dunia, namaanisha kila kinachokuzunguka. Kuanzia watu, mimea, ardhi, wanyama na chochote kilichopo duniani ambacho kinahusika na wewe hapo ulipo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog