Kusudi la maisha halijawahi kuteseka,
Ni kweli changamoto na vikwazo vingi vipo kwenye safari ya maisha, lakini havipaswi kuwa chanzo cha mateso.
Ukiiangalia dunia jinsi ilivyo, hakuna namna yoyote imejipanga kuwatesa watu. Lakini watu wanateseka kila siku, kwa sababu wanachagua kujitengenezea mateso wao wenyewe.
Yaani ni sawa na kuwe na chumba, ambacho mtu angeweza kukaa na kukifurahia, lakini yeye mwenyewe anaamua kukigeuza kuwa gereza na kujifungia ndani yake.

Watu wanajitengenezea mateso pale wanapojitengenezea tabia ambazo zinakuwa mzigo kwao baadaye. Tabia kama ulevi, mwanzo watu huanza nayo kama kitu kizuri na chenye raha, lakini baadaye hugeuka kuwa mateso na utumwa. Pale ambapo mtu hawezi kabisa kuacha ulevi.
Watu wanajitengenezea mateso pale wanapoweka maisha yao kwenye mikono ya wengine. Pale wanapoamini kwamba bila ya watu fulani maisha yao hayawezi kwenda. Wanampa mtu huyo nafasi ya kufanya chochote kwenye maisha yao, na hilo linatengeneza maisha ya mateso.
Watu wanajitengenezea mateso pale wanapojaribu kuitabiri kesho, pale watu wanapojaribu kuangalia namna mambo yanavyoenda leo na kujitengenezea kanuni kwamba yataendaje kesho. Kisha wanaweka matumaini yao juu ya utabiri huo, kesho kinatokea kitu tofauti na wanaumia sana.
Watu wanajitengenezea mateso pale wanapotafuta njia ya mkato ya mafanikio. Pale wanapotaka kupata kitu bila ya kutoa kitu, pale wanapotaka mafanikio makubwa lakini hawapo tayari kuweka kazi kubwa. Wanajikuta wameingia kwenye mambo yasiyo sahihi na yanayowatesa kwa maisha yao yote.
Zipo njia nyingi sana ambazo watu wanazitumia kujitengenezea mateso, kwa mifano hii michache, unaweza kuona njia nyingine ambazo wewe mwenyewe unajitengenezea mateso kwenye maisha yako.
SOMA; UKURASA WA 357; Maumivu Na Mateso.
Neno ni moja rafiki, ACHA, acha kabisa kujitengenezea mateso, acha kabisa kufanya kitu chochote ambacho siyo sahihi, ambacho hakiendani na sheria za asili, ambacho hautakuwa tayari kuandikwa kwenye vyombo vya habari kwamba umefanya. Na pia usifanye kitu chochote ambacho baadaye huwezi kuacha, kwa sababu chochote ambacho huwezi kuacha kinakuwa kimekutawala, na chochote kinachokutawala kitakutesa.
Acha kujitengenezea mateso, maisha hayajawekwa ili tuteseke, bali tuyaishi na tuyafurahie.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog