Mwandishi Brian Tracy kwenye kitabu chake cha THE PSYCHOLOGY OF SUCCESS anasema kwamba watu ambao hawajafanikiwa wana tatizo kubwa sana. Wakipata kitu wanaona ni bahati, na wakishindwa au kukosa kitu basi wanaona ni bahati mbaya au kisirani kwao.
Kwa njia hiyo, hawajifunzi na wala hawapati mbinu bora za kupata kile wanachotaka.
Ukiangalia sehemu kubwa ya watu wanaendesha maisha yao kwa njia hii. Wakifanikiwa basi ni bahati na wakishindwa basi kuna watu wa kuwalaumu, kuanzia mazingira, watu wengine na hata vitu visivyofaa kulaumiwa.

Leo nataka nikushirikishe kuhusu DARASA LA KUSHINDWA KWAKO.
Ninachotaka kukuambia hapa ni kwamba, unaposhindwa kwenye jambo lolote, unahitaji kuchukua darasa la uhakika la kushindwa huko. Unahitaji kukaa chini, ukiwa na utulivu, kalamu na kijitabu chako na uanze kujifunza kutokana na kushindwa kwako.
Unahitaji kuandika kwa kina jinsi hali ilivyoenda mpaka ukafikia kushindwa au kukosa ulichotaka. Halafu uanze kuandika wapi ungefanya tofauti, au kipi ungeboresha zaidi ili kuleta matokeo bora zaidi.
SOMA; UKURASA WA 1014; Dhambi Kubwa Siyo Kukosea, Bali Kutokufanya Kabisa…
Zoezi hili litakufungua uone wapi unapokosea ili usirudie tena makosa hayo baadaye. Zoezi hili litakufanya ubebe jukumu la mafanikio yako na uache kuwalaumu wengine kwa mambo ambayo umesababisha wewe mwenyewe.
Chukua darasa kwenye kushindwa kwako, na utaona wazi wapi ambapo umekuwa unakosea au kuanguka, kisha uweze kuchukua hatua za kurekebisha hilo.
Kadhalika, chukua darasa kwenye mafanikio yako, kwa lolote unalofanikiwa au kupata, kaa chini na andika kila hatua uliyochukua, kisha fikiria kipi ungeweza kuboresha zaidi.
Naamini unajua kwamba haijalishi umefanikiwa kiasi gani, bado kuna namna unaweza kuwa bora zaidi. Fanya hivyo kwenye mafanikio yako, na utaziona fursa za kufanikiwa zaidi na zaidi.
Hakuna kinachotokea kwa bahati nzuri au mbaya, na wala huna kisirani cha aina yoyote, bali kila kinachotokea, kwa namna moja au nyingine umekisababisha wewe mwenyewe. Anza kuchukua hatua kwa upande wako na mambo yatakuwa bora sana kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog