Be careful to leave your sons well instructed rather than rich, for the hopes of the instructed are better than the wealth of the ignorant. – Epictetus
Hongera rafiki kwa siku hii nyingine nzuri na ya kipekee sana ya leo.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo mazuri sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WAJENGEE MISINGI, SIYO KUWAPA FEDHA PEKEE…
Kila mzazi anapenda watoto wake wawe na maisha mazuri,
Na wazazi wengi wamejitoa kuhakikisha maisha ya watoto wao yanakuwa bora hata kama wao hawatakuwepo duniani.
Lakini njia wanayotumia kufikia hilo, kwa wengi imekuwa siyo sahihi, imekuwa njia inayowatengenezea watoto matatizo makubwa kuliko kuwasaidia.
Kwa mfano wazazi wengi wamekuwa wakiwaandalia watoto wao fedha na mali, na kwa matumaini kwamba zitawasaidia kuendeleza maisha yao.
Lakini wamekuwa hawawapi na kuwafundisha kwa vitendo watoto hao misingi ambayo wao wameishi na kuweza kufika pale.
Hivyo watoto wao wanaona mali zile ni rahisi kupatikana na kazi kubwa kwao ni kutumia.
Ndiyo maana kila mara tumekuwa tunaona mali zinazoachiwa watoto zikipotea haraka pale wazazi wanapofariki. Ni kwa sababu watoto wanakuwa na mali lakini hawana misingi. Na mali au fedha bila misingi, ni hatari kuliko kukosa fedha kabisa.
Kitu kikubwa kabisa tunachoweza kufanya kwa watoto wetu, kuwasaidia kuwa na maisha bora, ni kuwawezesha kujenga misingi imara ambayo wataiishi kipindi chote cha maisha yao.
Kuhakikisha wanaelewa misingi ya upatikanaji na ukuzaji wa mali.
Na hapa tutakuwa tumewapa kitu kikubwa na kidumucho kwenye maisha yao yote.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha