We should not moor a ship with one anchor, or our life with one hope. – Epictetus
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MELI YENYE NANGA MOJA…
Hakuna mtu yeyote, mwenye akili zake timamu atakayeweka meli ambayo imesimamishwa na nanga moja.
Chochote kinaweza kutokea na mambo yakaenda tofauti na mtu alivyotarajia.
Kadhalika kwenye maisha yetu, haipaswi maisha yako yote ukayaweka kwenye tumaini moja, hasa kwa vile vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu.
Chochote kinaweza kutokea kwa ulipoweka tumaini lako na mambo yakaenda tofauti na ulivyotarajia.
Kama ambavyo meli itasimama imara ikiwa na nanga nyingi, ndivyo maisha yako yanavyokuwa imara ukiwa na matumaini mengi.
Usikubali kabisa mtu mmoja au kitu kimoja kiwe na nguvu ya kuharibu kabisa maisha yako.
Mara zote kuwa na mpango mbadala, mara zote kuwa na njia mbadala.
Hata kama umeshawishiwa na kujishawishi kiasi gani kwamba mambo yataenda vizuri, tumaini linapokuwa sehemu moja, ni kujiandaa kushindwa au kukosa.
Ukawe na siku bora sana ya leo mwanamafanikio.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha