Kila wakati unao uhuru wa kuchagua maisha unayaotakiwa kuishi. Katika uchaguzi huo hakuna anayeweza kukuamulia ya kwamba wewe uishi maisha ya aina gani. Mara nyingi uamuzi wote wa uchaguzi unaotakiwa kuufanya upo mikononi mwako,

Hata hivyo kwa bahati mbaya sana watu wengi huamua kuchukua uchaguzi rahisi kwenye maisha yao. Ni wachache tu, ambao huamua kuchukua uchaguzi mgumu na ambao wanaoutumia kwenye maisha yao na kuwasaidia.

Kwa nini swala la uchaguzi rahisi linakuwa linashika kasi, hii ni kwa sababu uchaguzi rahisi, ni rahisi sana pia kutekelezeka na unakuwa hakuna ugumu wowote. Hakuna kufikiria sana hasa pale unapofanya uchaguzi rahisi tofauti na uchaguzi mgumu.

Kwa mfano, kulalamika kwako inaweza ikawa ni kitu rahisi sana, lakini jiulize kwa kulalamika huko unatatua changamoto ipi, hapa jibu ni hakuna. Kama ni kulalamika utaendelea kulalamika lakini hakuna changamoto unayoitatua.

Achana

Lakini, ukija kuangalia kwa upande wa pili, tuchukulie ukachagua kutatua changamoto badala ya kulalamika, inaweza ikawa ni kazi ngumu sana, hata hivyo kupitia kutatua changamoto hizo kuna utofauti wa maisha ambao utauleta tena kwa uwazi.

Pia kufanya uchaguzi wa kuchelewa kuamka ni kitu rahisi sana kwa wengi ukitofautisha na kuwahi kuamka. Sasa tuangalie kipi unachokipata kikubwa kwa kuchelewa kwako kuamka, utakuta hakuna zaidi ya kujichelewesha kupanga mipango yako mapema ya kukusaidia.

Kwa mifano hiyo michache, inazidi kuonyesha kwamba kwa wote ambao wanaendelea kufanya uchaguzi rahisi kwenye maisha yao, wanaendelea kuwa watumwa wa uchaguzi wao huo ukilinganisha na watu ambao wanafanya uchaguzi mgumu.

Mara nyingi tumekuwa tukiambiwa rahisi ni gharama, na ni ukweli mtupu. Hata uchaguzi rahisi ambao unaufanya kweye maisha yako unaharibu na kubomoa maisha yako kwa nguvu sana kuliko ambavyo ungefanya uchaguzi mgumu.

Unachotakiwa kuelewa usiogope kuchukua uamuzi mgumu, fanya uamuzi mgumu ambao mwisho wa siku utakusaidia wewe kuweza kutatua changamoto zako na kuishi maisha ambayo unayataka.

Kinyume cha hapo kama wewe kila siku na kila wakati unataka uchaguzi rahisi, utakukwamisha, maana huo ndio uchaguzi ambao kila mtu anaoufanya na ndio unaopelekea maisha ya wengi kuwa magumu sana.

Sitaki maisha yako yaendelee kuwa magumu, kipo kitu ambacho unatakiwa kukibadili. Na mabadiliko hayo ambayo unaweza ukaanza kuyafanya ni kubadili kupitia maamuzi yako. inabidi uwe makini na maamuzi yako.

Hapa unachotakiwa kuchunga sana ni juu ya maamuzi unayoyachukua kila siku, unatakiwa kukagua maamuzi au uchaguzi wako ni uchaguzi wa aina gani? Kama ni uchaguzi rahisi basi achana nao maana utakuharibia maisha huo.

Kama nilivyoanza makala haya, uamuzi unabaki kuwa mikononi mwako ni uchaguzi upi uutumie kuendeshea maisha yako, uchaguzi rahisi au uchaguzi mgumu. Ila uelewe tu, kama utaendele kufanya uchaguzi rahisi hutaweza kufanikiwa kamwe.

Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatumia.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com