Kuna mambo madogo madogo ambayo tunayafanya kila siku, ambayo hayana hatia kabisa, yaani ni mambo ya kawaida mno, ambayo haitujii kwenye akili zetu kwamba yanaweza kuwa na madhara makubwa kwenye maisha yetu.

Kwa mfano kuianza siku yako kila siku kwa kusikiliza habari na matukio mbalimbali ambapo nyingi huwa ni hasi. Ni kitu ambacho unaweza kuona cha kawaida kabisa, ambacho kila mtu anafanya. Lakini kadiri unavyoendelea kufanya hivyo, ndivyo unavyotengeneza mawazo na mtazamo hasi juu ya maisha kwa ujumla. Kidogo kidogo unaanza kuona mambo hayawezekani na kuona kila kitu na kila mtu ni mbaya. Unajikuta unashindwa hata kuchukua hatua ndogo kwa kuona hauwezi kufanikishwa. Hatua ndogo ambazo hazikuonekana kuwa na hatia zinakuwa zimefikia kuzalisha hatua kubwa sana.

siyo ajali

Mifano ipo mingi, kwenye matumizi yetu ya muda, fedha, mahusiano yetu na wengine, yapo mambo tunayoweza kuona ni madogo na hayana madhara, lakini mwishoni yakaleta madhara makubwa.

SOMA; UKURASA WA 971; Ubaya Ni Pale Vinapotokea Kidogo Kidogo…

Na madhara siyo lazima yawe chanya, matendo madogo chanya yanaweza kuzalisha madhara makubwa sana chanya. Kwa mfano mtu anayeweka akiba ndogo kabisa ya shilingi elfu moja kwenye kipato chake, ni kiwango kidogo ambacho kwa wengi wanaamini hakiwezi kutengeneza utajiri mkubwa. Lakini anayeanza hivyo na akafanya hivyo kwa muda mrefu, anaweza kupiga hatua kubwa sana kifedha baada ya muda. Siyo tu kile kiwango kidogo kinamsaidia, bali ile tabia anayokuwa ameshaijenga inazalisha madhara makubwa zaidi kwenye kile anachofanya.

Nakukumbusha hili rafiki yangu ili uache kuchukulia poa chochote unachofanya kwenye maisha yako. Ukishaona kitu unakirudia rudia kufanya, kaa chini na angalia kwa mwenendo huo utafika wapi miaka 10 ijayo, kisha fanya mabadiliko pale inapobidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog