All cruelty springs from weakness. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UKATILI NI ZAO LA UDHAIFU…
Watu wote ambao wanafanya ukatili, ni watu dhaifu sana.
Kutokana na udhaifu wao, humaribu kuuficha kwa kufanya ukatili kwa wengine.
Au udhaifu wao unawafanya waone kila mtu ni mbaya kwao.
Au wanatumia ukatili kama kitu cha kuficha udhaifu wao.
Watu dhaifu ni watu hatari, kwa sababu huumiza wengine kuficha udhaifu wao.
Asubuhi ya leo tafakari hili kwa njia hizi mbili;
Moja; je una udhaifu wowote ambao umekuwa unajaribu kuuficha kwa kuwaumiza wengine? Huenda hujui kama unafanya hivyo, ndiyo maana ni muhimu utafakari hili.
Mbili; je kuna mtu yeyote unamwona ni katili au anafanya mabaya kwako au kwa wengine? Hebu mwangalie kwa undani na utaona ni kitu gani anajaribu kuficha, utaona ni namna gani ana udhaifu mkubwa ndani yake.
Tusikubali udhaifu wetu uwe maumivu kwa wengine, na wala udhaifu wa wengine uwe maumivu kwetu.
Nakutakia siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha