Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza sehemu kubwa yenye idadi ya  wafungwa wengi tofauti na magereza tunazozifahamu, hivyo basi,  karibu tujifunze.

Rafiki, tumezoea kuona kuwa wafungwa mara nyingi huwa wanapatikana katika magereza zetu kama vile gereza la ukonga, karanga na magereza mengine yaliyoko karibu nawe. Kumbe basi, licha ya kuwa na magereza hizo lakini watu wengi wanaishi maisha ya vifungo vikubwa zaidi ya wale ambao wako magerezani.

f898e-mitandao

Familia zetu zinawafungwa wengi, familia zetu zimekuwa na magereza zinazozalisha wafungwa. Watu wengi wafungwa na vifungo mbalimbali katika familia wapo wenye matatizo ya kila aina na kama kila nyumba ingeweza kuweka mambo yao hadharani basi ndiyo ungejua katika familia kuna wafungwa wengi kuliko magereza. Ni wazi kwamba familia ndiyo sehemu yenye wafungwa wengi kuliko hata magereza tunazozifahamu.

Leo nakwenda kukushirikisha magerza hiyo ambayo inadadi kubwa za wafungwa kuliko hata hizo magereza kubwa unazozifahamu katika jamii yako unayoishi. Sehemu ambayo ina idadi kubwa za wafungwa na imekuwa ni gereza ni familia na wafungwa wakubwa katika magereza hizi ni sisi wenyewe.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Born To Win (Umezaliwa Kushinda, Ijue Siri Yako Ya Mafanikio)

Mpendwa msomaji, wako wanaoishi katika familia hawajui kitu kinachoitwa upendo, na kama mtu akikosa upendo ni wazi kabisa amekosa maisha kwa sababu upendo ndiyo maisha, ndiyo hazina pekee ambayo inatufanya tuendelee kuishi na kutegemeana kila siku. Watu wamekosa amani katika familia hivyo familia zimegeuka kuwa magereza za watu waliokosa amani. Bila amani hatuwezi kufanya shughuli yoyote ile ya kimaendeleo, bila amani katika familia zetu ni wazi kama tuko kwenye vifungo vinavyotukosesha furaha ya kuendelea kuishi.

Watoto wanaishi maisha ya hofu,baba na mama wanaishi maisha ya kila mtu na hamsini zake hivyo familia imekuwa ni magereza iliyokosa utulivu. Magomvi yanatawala hivyo badala ya kujenga familia tunakuwa tunajenga magereza na hivyo wafungwa wakubwa tunakua ni sisi wenyewe tunaopatikana katika hizi familia.

Familia zetu zimekosa uhuru wala hakuna haki hivyo mateso yanayopatikana katika baadhi ya familia tunaweza kusema ni magereza na wafungwa wenyewe ndiyo hao wahanga wa familia. Rafki, ukijaribu kuchunguza katika familia nyingi kuna matatizo mengi ambayo yanajenga magereza na kuongeza wafungwa kila siku. Wako watu wanaopitia katika magumu katika familia zao hivyo hata ukiwaambia wanaishi kwenye vifungo hawawezi kukataa hata mara moja.

Watu wanaishi maisha wasiyoyataka, wanaishi maisha ambayo siyo yao, hivyo wamekuwa wanabeba mizigo mikubwa ya kuishi maisha ya wengine huku ya kwao hawajawahi kuishi hata siku moja. Wako wanaoshi katika magereza za kutoonja huruma ya kusamehewa wala kusamehe, watu wanaishi kwa visasi, chuki , wivu na hivyo basi mambo haya yote huwa yanazaa mauti makubwa.

SOMA; Huu Ndiyo Wakati Sahihi Wa Kutua Mizigo Tuliyobeba Kwenye Mioyo Yetu.

Hatua ya kuchukua leo, ni wakati sasa wa kutoka katika vifungo mbalimbali na kuwa huru. Maisha ambayo hayakupi kile ambacho unakitaka siyo maisha ya kuishi hata siku moja. Hujaletwa duniani kuja kuteseka bali kufurahia maisha hivyo ni wakati wako sasa wa kufanya mageuzi na kubadili kile kinachokufanya uende kwenye magereza na kuwa mfungwa wa kujitakia.

Mwisho, mtu pekee wa kukutoa katika magereza ambayo uko kadiri ya maisha unayoishi ni wewe mwenye hivyo kaa chini na amua kubadili maisha yako leo.  Wafungwa wanaopatikana katika familia zetu ni sisi wenyewe hivyo kila mtu anayajua maisha anayoishi na changamoto anazopitia. Familia zetu zigeuke kuwa nyumba za amani na siyo sehemu za vifungo.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.