Anger: an acid that can do more harm to the vessel in which it is stored than to anything on which it is poured. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera rafiki yangu kwa siku hii bora na ya kipeke sana kwetu. Ni nafasi nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari USITUNZE TINDIKALI, ITAKUUNGUZA…
Tindikali huwa na sifa moja kuu, ni kali na inaunguza chochote ambacho kinaibeba. Hivyo ukiweka tindikali kweye chombo, chombo hicho kinaungua. Hata kama ni chombo kigumu kiasi gani, kitaungua kidogo kidogo.
Hivi ndivyo ilivyo kwa hasira.
Hasira ni sawa na tindikali, wewe unayeibeba hasira ndiye unayeumia kuliko yule unayemkasirikia.
Wakati wewe unajiumiza na hasira zao juu ya kitu ambacho mtu amefanya au kusema, mwenzako anakuwa anaendelea na maisha yake, tena huenda hata akawa hajui au hakumbuki amewai kukufanyia jambo la kukukasirisha.
Kama mtu amekuudhi, hili hutokea mara kwa mara, mweleze wazi wapi amekuudhi, kipi alichofanya hujapendezwa nacho. Na baada ya hapo malizana na jambo hilo.
Usiendelee kubeba chochote moyoni mwako, hasa kwa yale ambayo wengine wamekukosea.
Usikae na hasira ndani yako, ni kujiumiza wewe mwenyewe na siyo yule unayemkasirikia.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha