Kama kuna neno moja ambalo limetumika vibaya mpaka hata kupoteza kabisa maana yake, ni neno fursa. Kila siku watu wapo ‘bize’ kutafuta na kukimbizana na fursa.

Na kwa namna fursa hizi zinavyoonekana na kuchukuliwa, zinavutia na kutamanisha mno. Mtu anavutiwa kufikiri kwamba kama asipoingia kwenye fursa fulani basi hawezi kufanikiwa.

Wengine wanaaminishwa kwamba wakichelewa kuchukua hatua kwenye fursa wanayoiona sasa, wataipoteza milele na hawatafanikiwa.

Kila Changamoto

Na mbaya zaidi, ndani ya hizo zinazoonekana fursa, kuna utapeli mwingi na uongo mkubwa sana. Wengi huoneshwa na kuona yale matokeo ya mwisho, ambayo ni matokeo mazuri, mafanikio makubwa, fedha nyingi.

Lakini huwa hawaoneshwi mchakato mzima unaopelekea matokeo hayo. Mbaya zaidi hawaambiwi uwezekano mkubwa wa kushindwa, wa kutokupata matokeo hayo bora.

Hivyo watu wanaingia kwenye mtazamo huu wa kusaka fursa, wakiwa na imani kwamba wakiingia kwenye fursa fulani, basi maisha yao yamenyooka na mafanikio ni wazi wazi.

Wanapoingia kwenye fursa hiyo, wanakuta mambo ni tofauti, wanaanza kukutana na ugumu, wanakutana na changamoto. Kabla hawajakaa chini na kuzitatua, wanasikia kuna fursa nyingine nzuri zaidi, fursa rahisi zaidi na hiyo ni bora kuliko zote, ukichelewa unaikosa.

Watu wanaacha kile walichokuwa wanafanya, ambacho hata hivyo kimeshakuwa kigumu na kuingia kwenye fursa ile mpa. Hapa ndipo hatari kubwa ilipo kwa sababu mtu anajikuta akibadili fursa kila mara, anapokuja kustuka muda umepita na hakuna kikubwa alichopata.

SOMA; UKURASA WA 994; Siyo Mwanzo Na Wala Siyo Mwisho…

Ninachotaka kukukumbusha rafiki yangu;

  1. Hakuna fursa yoyote ambayo ni rahisi, hata watu wakushawishi na kukuonesha kuwa ni rahisi kiasi gani, kila kitu kinahitaji kazi na muda. Lazima uweke kazi ya kutosha na itakuchukua muda kufika kule unakoona wengine wamefika.
  2. Hakuna fursa ambayo ndiyo hiyo tu itakuletea mafanikio, achana na habari kwamba ukikosa fursa fulani basi maisha yako yameshindwa. Fursa zipi nyingi, ni wewe kuchagua unaweza kuweka kazi na uvumilivu eneo gani kisha kuchukua hatua.
  3. Hakuna fursa yoyote ambayo ukikosa huwezi kuja kuipata tena, labda fursa ya kuishi tu. Fursa nyingine zipo tu, kama alivyowahi kusema Richard Branson – ‘fursa ni kama basi la abiria, ukikosa moja, kuna jingine linakuja’
  4. Kukimbizana na kila aina ya fursa hakuwezi kamwe kukufikisha kwenye mafanikio. Unahitaji kuchagua fursa moja na kuweka juhudi zako kwenye fursa hiyo ili kufanikiwa.
  5. Waogope sana watu ambao kila wakati wanakuletea taarifa ya fursa mpya. Ukichunguza kwa umakini utagundua wananufaika zaidi na taarifa za fursa wanazokupa kuliko kunufaika na fursa yenyewe.
  6. Mwisho kabisa, usitafute njia ya mkato ya mafanikio, kila kitu kinahitaji kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog