Whoever does not regard what he has as most ample wealth, is unhappy, though he be master of the world. – Epictetus
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Hongera pia kwa mwaka huu 2017 ambao unakwenda kuisha leo. Nina imani ni mwaka ambao umeweka alama fulani kwenye maisha yako.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; UTAJIRI ULIONAO…
Popote ambapo unataka kufika kwenye maisha yako,
Mafanikio yoyote unayoyafikiria,
Hatua zozote unazotaka kupiga,
Utaanzia hapo ulipo sasa, ndiyo, hapo ulipo.
Hii ina maana kwamba, namna unavyochukulia hapo ulipo, kuna mchango mkubwa sana kwa hatua unazoweza kupiga.
Kama unachukulia hapo ulipo kama mtu wa kukosa, mtu usiyestahili, basi utakuwa na kila sababu ya kuendelea kukosa na kutostahili.
Lakini kama utachukulia kama mtu ambaye tayari umebarikiwa, kama utathamini kila ulichonacho, basi utakuwa na hamasa ya kuchukua hatua na utaziona hatua zaidi za kuchukua.
Kila ulichonacho sasa, ni utajiri ambao unaweza kuzalisha utajiri zaidi.
Pumzi uliyonayo ni utajiri mkubwa, bila ya kuwa hai huwezi kufanya chochote.
Afya bora na nguvu ulizonazo ni utajiri wa kipekee, bila ya afya huwezi kuchukua hatua yoyote.
Unaowajua na wanaokujua ni utajiri mkubwa, hao ndiyo watakaokupa kile unachotaka.
Usikubali kabisa kuwa na fikra za uhaba, fikra za kuona umekosa, hustahili au unaonewa.
Una utajiri wa vitu mbalimbali, ni wewe kujua namna ya kuugeuza kukupa utajiri mwingine unaohitaji zaidi.
Lazima uanzie hapo ulipo sasa kuweza kupiga hatua zaidi.
Asubuhi ya leo tafakari kila utajiri ulionao.
Kisha chukua dakika chache kuona ni namna gani unaweza kutumia kila utajiri ulionao kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Ukawe na siku njema sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha