Leo ni siku ya mwisho kabisa ya mwaka huu 2017. Hatutakuwa na mwaka mwingine kama huu kwa kipindi chochote hapa duniani. Na yale ambayo tumefanya au kutokufanya katika kipindi cha mwaka huu, yametuandaa kwa namna mwaka 2018 utakavyoenda.

Kila mwaka kuna mengi tunajifunza, kupitia yale tunayofanya, yale wanayofanya wengine na hata yale tunayojifunza kwa kusoma na njia nyingine. Ni muhimu kila mwisho wa mwaka kama hivi kupata muda wa kutafakari mwaka wako uliendaje na namna gani unakwenda kuwa bora zaidi kwa mwaka unaofuatia.

Nimekuwa na utaratibu wa kujipa likizo kila mwisho wa mwaka, likizo ya kujifunza na kutafakari kwa kina kila ambacho nimefanya kwa mwaka husika na namna gani napiga hatua zaidi kwa mwaka unaofuata. Hili ni zoezi linalohitaji kazi na kuwa mkweli kwako binafsi. Siyo zoezi la kujifurahisha kama wengi wanavyofanya wakati wa kuweka malengo. Lakini ni zoezi lenye manufaa makubwa.

Nilikushirikisha kidogo kuhusu likizo yangu hiyo kwenye makala hii, na pia nitaendelea kukushirikisha kadiri mwaka unavyokwenda, na kadiri nitakavyoendelea kuchukua hatua kuboresha zaidi huduma zangu.

2017 kwenda 2018

Leo nakwenda kukushirikisha mambo mbalimbali ambayo nimejifunza mwaka huu 2017. Mengine ni mapya, mengine nilishajifunza lakini mwaka huu niliyakumbuka kwa namna mambo yalivyokwenda.

Karibu kwenye mambo haya ambayo mwaka 2017 umenifundisha…

 1. Muda ni zaidi ya pesa, poteza milioni moja utaipata tena, poteza dakika moja na huwezi kuipata tena kamwe.
 2. Kupata saa moja kwa siku yako wewe binafsi, na kuitumia wewe bila ya usumbufu wowote, ni ushindi mkubwa sana kwenye maisha yako.
 3. Kila mtu anaweza kusoma kitabu kimoja kila mwezi, ni kiasi cha mtu kuamua kusoma kurasa kumi tu za kitabu kila siku, kitu ambacho kila mtu anaweza.
 4. Tunaishi kwenye dunia yenye usumbufu wa hali ya juu sana, bila ya kuwa makini, usumbufu huu utakupoteza.
 5. Kile ambacho watu wanasema huwezi au haiwezekani, wanachomaanisha ni kwamba wao hawawezi au walishindwa, ukiwasikiliza na wewe unashindwa kabla hata hujaanza.
 6. Watu wengi wanapenda kupata fedha, lakini hawapo tayari kufanya kazi, hivyo wanatafuta njia za mkato, ambazo hazijawahi kumnufaisha yeyote. Zinawapotezea muda mwingi.
 7. Ukifuata kundi kubwa la watu, lazima utapotea. Kwenye dunia ya sasa, hakuna kitu muhimu kama kufanya maamuzi yako mwenyewe, tena baada ya kufikiri kwa kina na bila ya hisia.
 8. Unaweza kupata raha sasa na ukateseka baadaye, au ukapata mateso sasa na kupata furaha baadaye, hakuna kukwepa, ni swala la kuchagua tu.
 9. Watu wengi hawaelewi msingi mkuu wa upatikanaji wa fedha, ambao ni kutoa thamani, hii inawapelekea kutapeliwa na hata kupoteza muda kwenye mambo yasiyo na maana.
 10. Utamjua mtu kwa uhalisia akiwa na vitu viwili; fedha na madaraka, kila mtu anaweza kuvumilia mateso, lakini mtu anapokuwa na fedha au madaraka, ndipo tabia zake zinaonekana wazi.
 11. Mitandao ya kijamii imekuwa usumbufu kwa watu wengi, watu wengi wamekuwa watumwa wa mitandao ya kijamii, wakiishi maisha ya kuigiza na kutokuwa na furaha.
 12. Unaweza kumdanganya kila mtu kwenye maisha yako, lakini huwezi kujidanganya wewe mwenyewe. Unaweza kujionesha utakavyo kwa nje, lakini unapokwenda kulala, unakutana na wewe kwa uhalisia, na hilo linawaumiza wengi sana.
 13. Habari hasi zinapendwa na kusambazwa kuliko habari chanja. Tunaishi kwenye zama ambazo habari sasa zinatufuata mpaka kitandani, ni masaa 24 kwa siku saba za wiki.
 14. Simu janja tunazotumia, ni moja ya kifaa chenye nguvu sana na pia chenye sumu kali. Kwa wengi wanakutana na sumu ya kifaa hichi, kwenye kupoteza muda kwa mambo yasiyo na maana.
 15. Kutegemea chanzo kimoja pekee cha kipato ni utumwa wa kujitakia, ni kuweka mustakabali wa maisha yako kwa mtu mmoja, ni hatari sana kwa maisha.
 16. Kukopa ni kuwatajirisha wengine, kukopa kwa ajili ya matumizi ambayo hayazalishi, ni maamuzi mabovu kabisa ambayo mtu anaweza kufanya kwenye maisha yake.
 17. Watu wengi, wananunua vitu ambavyo hawavihitaji, kwa fedha ambazo hawana, kuwafurahisha watu ambao hata hawajali. Hakuna utumwa mkubwa kwenye maisha kama kujaribu kumfurahisha kila mtu, kwa sababu mwisho wa siku hakuna unayeweza kumfurahisha.
 18. Uaminifu unalipa sana, uaminifu ni mtaji, uaminifu unaweza kukufikisha mbali sana.
 19. Uadilifu ni msingi muhimu kwenye maisha, bila huo, maisha yanaanguka.
 20. Bila ya nidhamu, hakuna chochote ambacho mtu anaweza kukamilisha, hasa kwa dunia ya sasa ambayo imejaa changamoto na vikwazo vya kila aina.
 21. Kuna watu ambao wanafanya kazi ili waonekane wapo kazini, na kuna ambao wanafanya kazi ili kutoa thamani kwa wengine. Wanaofanikiwa ni wale wanaotoa thamani.
 22. Kipato anachopata mtu ni sawasawa na thamani anayotoa kwa wengine, wenye vipato vidogo wanatoa thamani ndogo sana, ambayo pia inaweza kutolewa na wengine. Wenye vipato vikubwa wanatoa thamani kubwa, ambayo siyo rahisi kupatikana kila mahali.
 23. Afya ya mwili, akili na roho ni muhimu sana kwa maisha ya mafanikio.
 24. Kwenye mwili unahitaji kula vizuri, kufanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika.
 25. Kwenye akili unahitaji kujifunza kila siku.
 26. Kwenye roho unahitaji kusali na kutahajudi kila siku.
 27. Watu wanapenda sababu kuliko matokeo, wengi wapo tayari kutafuta kila aina ya sababu, ila tu wasitoe matokeo.
 28. Ukikutana na mtu anaongea sana, jua utendaji kwake ni mdogo. Kuwa makini na watu wanaoongea sana, na kuahidi mambo mengi, wanaficha udhaifu wao kwenye utendaji.
 29. Hakuna njia moja pekee ya kuelekea kwenye mafanikio, hakuna fursa moja pekee ya kumpa kila mtu mafanikio. Njia zipo nyingi, fursa zipo nyingi, ni wewe kuchagua.
 30. Kadiri unavyopiga hatua kwenye maisha, ndiyo unavyokutana na mambo magumu zaidi. Hivyo usitegemee mambo kuwa rahisi unavyofanikiwa, yanazidi kuwa magumu.
 31. Mpumbavu ni mtu hatari sana, unayepaswa kumjua na kumkwepa kwa haraka sana. Kwa sababu mpumbavu hana cha kupoteza, na huwa hajifunzi, hivyo chochote unachofanya kwa mpumbavu, ni kupoteza muda wako.
 32. Ukishajiona umefika kileleni, hapo ndipo unapoanguka.
 33. Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyoona mafanikio makubwa zaidi yaliyopo mbele yako.
 34. Ukishaona unajua kila kitu, basi jua hakuna unachojua.
 35. Maisha yangekuwa rahisi, kusingekuwa na changamoto yoyote, kila kitu kingekuwa kinapatikana kwa urahisi, hivi unafikiri maisha yangekuwa na maana gani?
 36. Kucheza kamari(betting) na bahati nasibu kwa mategemeo ya kupata fedha za kuendesha maisha ni jambo la hovyo sana ambalo mtu anaweza kufanya. Cha kushangaza hii nayo imekuwa fursa, ni hatari sana kwenye ustawi wa uchumi kwenye jamii nzima.
 37. Mambo yanapokuwa magumu, watu hufikiri zaidi, na wale wanaofikiri sawasawa, wanaushinda ugumu.
 38. Usomaji wa vitabu, ni njia rahisi, nafuu na ya uhakika ya kuiba maarifa na uzoefu wa wengine na kuweza kuutumia kwenye maisha yako. Ukisoma vitabu vizuri ni kuvielewa ni sawa na kukutana na waandishi na wakakushauri moja kwa moja.
 39. Mabadiliko yoyote ni magumu sana mwanzoni, na yanachukua muda mpaka kuzoeleka, wengi hawayawezi na wanaoenda nayo wanafanikiwa.
 40. Kila kitu kinaanzia kwenye fikra zetu, huwezi kubadili chochote kama hutabadili fikra zako.
 41. Ukiruhusu watu wakuzoee sana, wanakuchukulia kawaida na wanakudharau, kulinda heshima yako kwa wengine, punguza sana mazoea na wengine.
 42. Utajiri hautengenezwi na kipato, bali kile ambacho mtu anafanya na kipato chake. Mtu anaweza kuwa na kipato kikubwa, akatumia chote na kukopa, huyu ataendelea kuwa masikini. Mwingine anaweza kuwa na kipato kidogo akatumia kiasi na kuweka akiba kiasi, ambayo anaiwekeza, huyu atakuwa tajiri.
 43. Ukifanya chochote unachofanya, kwa misingi ya kawaida tu, ukawa na msimamo na ukawa mtu unayeweza kutegemewa, utapiga hatua sana. Kwa sababu wengine wote wanafanya chini ya kiwango, wanafanya kwa mazoea.
 44. Watu wanapenda kuongozwa, watu wanatafuta kiongozi makini wa kuwapeleka mbele zaidi, ukiwa kiongozi bora, utapata wafuasi wengi, huhitaji hata kuwatafuta, wao watakutafuta wewe.
 45. Unapata watu unaowastahili, na wanaoendana na wewe. Kama unalalamika kwamba watu ulionao siyo waaminifu na hawajitumi, kwa hakika hivyo ndivyo ulivyo wewe, ndiyo maana umewavutia na unaweza kuwavumilia.
 46. Usipoweka viwango vyako kwenye maisha, utaishi kwa viwango vya wengine na siku zote maisha kwako yatakuwa magumu.
 47. Kitu chochote cha bure, kina gharama kubwa ndani yake, kama ulivyo ushauri wa bure, hautakugharimu chochote mpaka pale utakapoanza kuutumia.
 48. Watu wengi wanaoshabikia na kushauri mambo, hata hawayajui kwa undani, wamesikia na wao wanasema. Kamwe usifanye maamuzi ya maisha yako kwa ushauri wa wengine, upokee lakini fanya utafiti wako kwa kujifunza na utajifunza mengi zaidi.
 49. Usiingie kwenye vita na yeyote, usiwe na mapambano na mtu yeyote, usijenge uadui na watu. Lakini kama hayo yote yatashindikana, basi pigana vita ambayo una uhakika wa kushinda, vinginevyo, kubali kushindwa kabla hata ya vita, kwa sababu hakuna vita ambayo huwa inamwacha mtu salama.
 50. Hakuna jambo lolote ambalo tuna uhakika nalo kwenye maisha, labda kifo pekee. Hakuna yeyote anayeweza kuitabiri kesho. Hivyo chochote unachotaka kufanya, anza kufanya sasa, usisubiri mpaka uwe na uhakika.
 51. Muda pekee wa kuishi maisha yako ni sasa, jana ilishapita, huwezi kubadili chochote, kesho bado haijafika, huwezi kuibadili kwa vyovyote, lakini sasa, hapo ulipo, ndiyo wakati sahihi kwako kuishi.

Hayo ni machache niliyoweza kukushirikisha leo, kati ya mengi sana ninayoendelea kujifunza kila siku. Tutaendelea kushirikishana kwenye makala mbalimbali nitakazokuwa nakuandalia kwa mwaka 2018.

Heri ya mwaka mpya 2018, ukawe mwaka wa wewe kuchukua hatua ili kuweza kufanikiwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog