Kwenye maisha, zipo ramani ambazo tayari zimeshatengenezwa, ramani za kila eneo la maisha yetu. Kila kitu cha kufanya ili mtu aweze kufika hatua fulani ya maisha yake.

Ramani hizi tumekuwa tunafundishwa tangu tukiwa watoto na kuhakikisha tunazielewa ili mambo yetu yaende vizuri.

Japokuwa ramani ni nzuri, hasa kwa mtu asiyejua namna ya kufika kule anakotaka kufika, ramani nyingi zina upungufu mkubwa wa kuamini kwamba kila mtu ana safari ya aina moja.

Ramani zilizotengenezwa ni kama vile watu wote wana safari moja na wote wanaelekea ukingo mmoja wa safari. Lakini sivyo ilivyo kwenye uhalisia.

tengeneza ramani

Kila mtu ana safari yake, na kila mtu ana njia tofauti ya kupita ili kufika kwenye safari hiyo.  Kwa hivyo kutegemea ramani moja iwafae watu wote, ni chanzo kikuu cha kukatishwa tamaa na kuangushwa kwa watu wengi.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Jinsi Ya Kuondoa Unafiki Kwenye Maisha Yetu, Kipi Unajifanya Huoni?

Lakini pamoja na changamoto hii ya ramani, bado siyo busara kukataa ramani zote na kutaka kutengeneza ramani yako peke yako. Ndiyo unahitaji kutengeneza ramani, lakini lazima uwe na pa kuanzia. Lazima ujue ramani nyingine zikoje, kisha utengeneze ramani inayokufaa wewe.

Hivyo ni muhimu kujua yale ambayo wengine wanafanyia kazi, yale ambayo watu wanategemea ufanye, halafu hapo sasa unaweza kutengeneza yaliyo bora zaidi kwako.

Kuna usemi kwamba kabla hujavunja sheria, kwanza ijue sheria hiyo. Kadhalika kabla hujatengeneza ramani yako mwenyewe, kwanza fuata ramani za watu wengine. Hizi zitakusaidia kuepuka changamoto za wazi na kupoteza muda kwenye kujaribu mambo yasiyo na manufaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog