Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Leo ni siku mpya, ya wiki mpya, mwezi mpya na mwaka mpya 2018.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kufanya yale ambayo tumekuwa tunapanga kufanya kwa muda mrefu.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; HERI YA MWAKA MPYA 2018….
Tayari tumeuanza mwaka mpya 2018,
Mwaka ambao kuna watu waliona ni mbali sana kufika, lakini sasa umeshafika.
Mabadiliko ya mwaka, ni mabadiliko ya tarehe, na yatabaki hivyo mpaka pale wewe utakapochukua hatua za kubadili maisha yako.
Maisha yako hayatabadilika chochote kwa sababu mwaka umebadilika, maisha yako yatabadilika pale unapoamua kuchukua hatua za dhati za kuyabadili.
Hivyo moja ya mambo makubwa ya kufanya 2018, ni kuchukua hatua na kubadili maisha yetu.
Yale ambayo tumejifunza mwaka 2017, yawe msingi kwetu kupiga hatua zaidi mwaka 2018.
Yale ambayo tumeshindwa mwaka 2017, yawe darasa kwetu la mafanikio kwa mwaka 2018.
Chochote ambacho tunajiambia kitakuwa bora mwaka 2018, kinaanza na sisi wenyewe.
Kama maisha yalikuwa magumu 2017, basi 2018 yatakuwa magumu zaidi.
Kama ulikuwa unamwona kila mtu ni mbaya kwako 2017, basi 2018 utakutana na wabaya zaidi.
Kile ulichokuwa unakiona 2017, ndiyo utaendelea kukiona 2018 mpaka pale utakapochukua hatua za kubadili fikra zako, mtazamo wako na hatimaye matendo yako.
Nikutakie mwaka bora sana kwao rafiki yangu, mwaka wa kufanya makubwa na kupiga hatua zaidi kimafanikio.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha