Ni hitaji la ndani la kila binadamu kupenda kuthaminiwa, kuonekana ni wa muhimu kwa chochote kile ambacho anakifanya.
Huu ni msukumo uliopo nyuma ya maamuzi ambayo wengi wanafanya, kuanzia mavazi wanayovaa, kazi na biashara wanazofanya, mali wanazomiliki na hata michango wanayotoa kwa wengine.
Hakuna ubaya wowote kwenye hilo, ila pale linapokuwa ndiyo msukumo pekee wa maisha ya mtu, ndipo tatizo linapoanza.
Pale mtu anapofanya kitu kwa sababu tu anataka kuonekana na wengine, anakuwa amechagua kupoteza muda na nguvu zake bure.

Hii ni kwa sababu watu wengi unaoweza kuwa unakazana kuwaonesha vitu fulani, hawana hata muda wa kuona kile unachotaka kuwaonesha, wapo ‘bize’ mno na mambo yao wenyewe.
Na wakati huo wewe unakazana kuwaonesha, unaacha kufanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako na hilo kupelekea wewe kushindwa kupiga hatua za maana kwenye maisha yako.
Hivyo badala ya kukazana kujionesha, ni vyema ukafanya kile ambacho ni muhimu kwako, ambacho kinatoka ndani yako, ambacho utafanya hata kama hakuna anayekuangalia.
SOMA; UKURASA WA 803; Wewe Ni Biashara…
Kwa kufanya kitu hicho, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya makubwa na hapo utaonekana. Na hapo ndipo penye siri kubwa kwa sababu wakati unakazana kujionesha hakuna anayekuona, lakini unapokazana kufanya kwa ubora, unaanza kuonekana.
Hivyo usipoteze nguvu zako kufanya lolote ili tu uonekane na wewe umefanya, utajiumiza sana. Badala yake weka nguvu zako kwenye kufanya yale ambayo ni muhimu kwako na watu wataanza kukuona, kwa namna ambavyo unafanya maisha yao kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog